Waislamu wote kwa madhehebu yao, hawana shaka iwapo nabii Isa aliyetanjwa ndani ya Qurán ndiye Yesu Kristo aliyetajwa ndani ya Biblia takatifu. Hata hivyo Baadhi ya Wakristo hawaamini ikiwa nabii Isa wa Qurán ndiye Yesu wa Biblia. Lengo langu siyo kujiingiza katika mjadala huo wa enzi na enzi,. Ninakubaliana na uelewa huo wa Waislamu kama ulivyodhihirishwa ndani ya Qurán yenyewe na mafundisho ya dini ya Kiislamu kwa ujumla. Hivyo ni kusudi la langu kuleta uelewa halisi wa nabii Isa (au Yesu) kulingana na vitabu vitakatifu, yaani Biblia, Qurán tukufu na Hadithi za mtume Muhammad (s.a.w)
Swali la Yesu kwa Wanafunzi wake.
Yesu alikuwa punde tu amekwisha kufanya muujiza wa kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili, kisa ambacho kimenukuliwa katika kitabu cha Luka 9:12-17. Ndipo baada ya muda punde akawauliza wanafunzi wake swali la mhimu sana katika maisha ya mwanadamu na pengine ndilo swali kuu kabisa ambalo hata leo linaendelea kuusumbua ulimwengu mzima. Katika kitabu cha Luka 9:18-20 tunasoma
“Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza. Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Wakamjibu wakisema, Yohana mbatizaji, lakini wengine Eliya; na wengine kwamba mmoja wapo wa manabii wa kale amefufuka. Akawaambia , nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu.”
Rafiki yangu mpendwa, ikiwa wewe Yesu angekuuliza swahi hilo hilo, je ungejibu vipi? Leo hii wengi wanatoa majibu tofauti kila mara wanapokabiliana na swali hili kama ilivyokuwa wakati huo wa Yesu. Wapo ambao wanaona kuwa Yesu alikuwa mtu miongoni mwa watu mashuhuri waliopata kuishi katika uso wa dunia, wengine husema ni miongoni mwa manabii wengi waliopata kuwepo katika dunia hii, weingine wanaona alikuwa mwalimu mashuhuri sana miongoni mwa waalimu waliowahi kuwako duniani, lakini sehemu kubwa ya watu huamini kama Petro kwamba Yesu ni Kristo wa Mungu na “Mwana wa Mungu aliye hai” Mathayo 16:16
Lakini kwanini watu huchanganyikiwa kiasi hicho kuhusu Yesu. Biblia iko wazi juu ya nini kilisababisha watu wachanganyikiwe kuhusu hali ya Yesu.
Kitabu cha Mathayo sura ya 16, kinaeleza mazingira yaliyopelekea Yesu awaulize wanafunzi wake swali hilo. Mafarisayo na Masadukayo hawakumwamini Yesu, walitilia mashaka huduma yake na kuongoza wengine pia kutia mashaka juu ya Yesu na ndipo tunasoma katika Mathayo 16:1
“Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni”
Maneno haya ya Mafarisayo na Masadukayo yaonyesha kwamba walitaka awaonyeshe ishara au muujiza ambao ungethibitisha kwamba yeye ametumwa kuja hapa ulimwenguni na kwamba anatoka kwa Mungu mbinguni. Mafungu yanayoendelea hapo yaonyesha kwamba Yesu alitarajia wangemwamini kutokana na miujiza mingi ambayo alikuwa ameitenda wakati huo, hata hivyo walizidi kukaza kutokuamini kwao wakidai ishara zaidi, ndipo akawajibu akisema
“Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara; wala hakitapewa, isipokuwa ishara ya Yona, akawaacha, akaenda zake” Mathayo 16:4
Yesu alikuwa na maana gani? Mafarisayo na Masadukayo walikuwa wameshuhudia ishara nyingi alizozitenda, bado walitaka ishara zaidi! Hii ina maana hata kama wangepewa ishara gani wasingemwamini Yesu. Kutaka kwao ishara zaidi kulionyesha kukosa kwao imani, na kama Yesu angefanya ishara zaidi ingemaanisha kuungana nao katika kutokuamini kwao na kutaka kuwaaminisha katika ishara na siyo katika Yesu mwenyewe. Hii yaonyesha hatari iliyopo ya mtu kuvutwa na ishara kuliko mtoa ishara mwenyewe.
Kisha Yesu aliwaonya wanafunzi wake akiwaambia katika Mthayo 16:6 akisema
“Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo”
Aya ya 12 inafafanua ni nini maana ya chachu hiyo
“Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mikate bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo”
Rafiki mpendwa unaona, kumbe mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo ndiyo hayo yaliyowachanganya watu wasiweze kumwamini Yesu kama alivyofunuliwa katika Maandko Matakatifu licha ya miujiza mingi aliyoitenda kuthibitisha utume wake. Hii inamaanisha kwamba iwapo hata leo watu wamechanganyikiwa juu ya Yesu ni kwa sababu kuna mafundisho au “chachu ya Mafarisayo na Masadukayo” wa kileo wanaochanganya watu.
Lakini kwanini tuchanganyikiwe, kwanini tushindwe kumfahamu Yesu kama alivyofunuliwa katika maandiko. Ikiwe wewe unaviamini vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu, ungana nami sasa tunapoyapitia maandiko yote tuone yanasema nini juu ya Yesu. Hatutakuwa na haja ya kuchanganyikiwa isipokuwa kwanza tumeshindwa kuyaamini maandiko. Na unajua shetani analijua hilo kwamba watu wakiamini Maandiko Matakatifu watamtambua Yesu ni nani na kumwanini kwa uzima wa milele. Ili awapotoshe na kuwakosesha uzima wa milele, atahakikisha anahafifisha imani yao juu ya Maandiko, kwani Yesu mwenyewe aliwahi kusema.
“Mwayachunguza maandiko, kwa sababu … mna uzima wa milele ndani yake, na hayo ndiyo yanayonishuhudia” Yohana 5:39.
“… Mwapotea kwakuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” Mathayo 22:29
“Akawaambia enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyosema manabii … akaanza toka Musa na manabii wote, akaweleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe” Luka 24:25-27.
Je ni vitabu gani ambavyo Yesu alisema vinamshuhudia yeye?
Au twaweza kuzipata habari za Yesu kutoka katika vitabu gani. Yesu mwenyewe anasema
“Kisha akawaambia, haya ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi. Luka 24:44
Hebu basi tujiunge sote kuangalia katika vitabu vya Taurati, Manabii na Zaburi ili tuweze kuwa na jibu sahihi juu ya swali hili kuu ambalo ninaamini hadi sasa Yesu anakuuliza moyoni, “wewe wanena kuwa mimi ni nani?”
Wahyi (Ufunuo) wa Mwenyezi Mungu katika Taurati, Manabii na Zaburi kuhusu Yesu.
“Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii walosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo ndani yao Roho wa Kristo aliyokuwa akionyesha alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. Mitume walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali walihudumu kwa ajili yenu katika mambo hayo ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo ambayo hata malaika wanatamani kuyafahamu.” 1Petro 1:10-12
Yesu Katika Torati ya Musa:
Neno hili torati ya Musa katika zama za Agano la Kale lilimaanisha vitabu vitano alivyoviandika mtumishi wa Mungu nabii Musa. Vitabu hivyo ni Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi na Kumbukumbu la Torati. Hivi vilijulikana kama vitabu vya sheria ama torati. Wote walioisoma vizuri torati hiyo, waligundua kabisa ya kwamba Yesu ni yeye “aliyeandikwa na Musa katika Torati na Manabii…” Yoha 1:45. Kwa hiyo basi ni vizuri kama tunataka nasi kuwa ha uhakika wa Yesu ni nani tuangalie Torati hii ya Musa.
Nabii Yakobo alieleza kuwa Yesu ni Nani?
Maneno ya wosia wa Yakobo kwa wanawe yanasomeka hivi;
“Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, wala mfanya sheria kati ya miguu yake, hata atakapokuja Yeye mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii” Mwanzo 49:10.
Yakobo anatabiri kwamba, kabila la Yuda lingeendelea kuwa na mtawala hata atakapokuja “Yeye Mwenye milki”. Ni nani huyu Mwenye milki na ambaye mtaifa wangemtii? Bila shaka mwenye milki ni mfalme, lakini huyu si mfalme wa kawaida tu, kwa sababu maandiko yanasema kwamba mataifa yote wangemtii, ikimaanisha kwamba ufalme wake ungekuwa ni ufalme wa dunia yote. Ili kufahamu jambo hili ni bora tuyageukie maandiko mengine ambayo yanatoa ufafanuzi wa nani atakuwa mfalme wa dunia yote.
Katika Qurán sura nzima ya kwanza (Surat-ul Faatihá) ni dua ambayo mwislamu anatakiwa kisoma kila wakati anapokuwa katika ibada yoyote. Mara tano kwa siku dua hii hufanywa na mwislamu. Dua hiyo inamlenga kumwabudu na kumwmba mwenye kumiliki siku ya malipo. Hii ndiyo sura ya kwanza ndani ya Qurán (Al-Faatihá) au Al-hamdu.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ
الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ,الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ
إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ, اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ
صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ ,غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu.
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu; Mwenye kumilki siku ya malipo. Wewe tu tunakuabudu, na wewe tu tunakuomba msaada. Tuongoe njia iliyonyooka, Njia ya ulio waneemesha, siyo ya waliokasirikiwa, wala waliopotea.
Hivyo ni wazi kwamba anayestahiki kuabudiwa ni Mwenye kumiliki siku ya malipo (yaani mwenye kumiliki siku ya hukumu). Je ni nani huyu Mwenyekumiliki siku ya malipo? ni kusudi letu mwisho wa kitabu hiki tuwe tumepata uhakika ni nani hasa anayemiliki siku ya malipo. Hii ni kwa sababu, ibada ya kweli inahusu kumwabudu Mwenyekumiliki siku ya malipo.
Mwenye Milki katika Mwanzo 49:10
Nimuhimu sana tuweze kufahamu ni nani aliye kusudiwa katika wosia wa Yakobo kwa wanae katika kitabu cha Mwanzo 49:10. Hii ni kwa sababu, ikiwa maneno hayo ni ya wosia bila shaka watoto wa Yakobo waliyazingatia sana na kungojea siku moja ambapo Yeye mwenyekuweka utawala wake juu ya mataifa wote atakapokuja. Hili lilibaki kuwa tumaini lao siku zote. Nabii wa Mungu Danieli yeye aliwahi kuoyeshwa katika njozi namna ambavyo huyo aliyetabiriwa na Yakobo atakavyotawala.
“Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Daniel 7:13-14.
Tutaangalia kwa undani zaidi huyu ambaye Danieli anamtaja kuwa ana mfano wa mwanadamu ambaye ndiye alipewa ufalme.
Yesu Mwenyewe aliyarudia maneno hayohayo akinena juu yake alisema;
“…lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu akija juu ya mawingu.” Mathayo 26:64.
Huku kuja na mawingu maana yake ni nini?
Yesu alielezea maana yake kwamba;
“Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake” Mathayo 16:27
“Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti chake cha utukufu wake na mataifa yote watakusanyika mbele zake…” Mathayo 25:31,32.
Mawingu hayo siyo mawingu ya kawaida isipokuwa ni mawingu ya wingi wa malaika watakaoambatana na Bwana atakapokuja mara ya pili. Na hapo ndipo atakaposimika ufalme wake wa milele. (Tutaangalia hoja hii baadaye)
Hivyo ni wazi kwamba huyo aliyeelezwa katika Danieli kwamba atakuja “na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa ni Yesu Mwenyewe.
Pia Maandiko katika Danieli hiyo yanasema kwamba ni mfano wa Mwanadamu.
Biblia iko waze kwamba Yesu ni mfano wa mwanadamu. Katika kitabu cha Wafilipi 2:5-12 tunasoma.
“Iweni na nia hiyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yu na namna ya Mungu, naye hakuona kuwa kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena alipoonekana kuwa ana umbo kama mwanadamu alijinyeyekeza akawa mtii hata mauti, naam mauti ya msalaba ...ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, vya duniani na vya chini ya nchi na kila ulimi ukiri ya kwamba YESU KRISTO NI BWANA,”
Zingatia katika kitabu cha Mwanzo 49:10 tumeona kwamba ufalme usingekoma katika kabila la Yuda hata ajapo mwenye miliki, yeye ambaye mataifa yote wange mtii. Ili kutimiza unabii huu Malaika alikuja kwa Mariam mamaye Yesu na kumwambia maneno yafuatayo.
“Tazama utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanaume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa mwana wa aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi Baba yake. Atamiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho” Luka 1:31-33.
Ni zipi sifa zingine za mtoto huyu mwanaume?
“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanaume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani…” Isaya 9:6-7.
Malaika wakiwapasha habari wachungaji wa kondoo siku ile Yesu alipozaliwa, walieleza sifa na kazi ambayo Yesu angeifanya.
“Maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa , kwa ajili yenu, Mwokozi, Ndiye Kristo Bwana”
Tayari hadi sasa tumeona mambo mengi kumhusu Yesu, Yeye ni Mfalme, Mungu mwenye nguvu, Mwokozi wetu. Bado Biblia inayo mengi ya kutueleza kuhusu Yesu. Ama kweli Biblia nzima haineni juu ya kingine chochote isipokuwa Yesu tu, ajenda nzima ndani ya Biblia ni Yesu pekee yake, ndiyo maana Yesu akasema katika Yohana 5:39 kwamba;
“Mwayachunguza maandiko… ninyi mnauzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia.”
Rafiki yangu ikiwa unayaamini maandiko ya Biblia basi soma kwa makini na utaelewa mengi kumhusu Yesu kwani maandiko hayo yanamshudhudia Yesu.
Nabii Baalamu alieleza kuwa Yesu ni Nani?
Balaamu alikuwa ni nabii miongoni mwa wana wa Mashariki. Hawa wana wa mashariki ni uzao wa Ibrahim kupitia kwa Hajiri (Wana wa Ishimaeli) na Ketura ambao baadaye walichanganyikana na uzao wa Esau (Soma Mwanzo 25:1-6; 36:1-43). Baalamu alionyeshwa katika njozi na kisha akasema.
“Namwona, lakini si sasa; Namtazama lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo; Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli… Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo,…” Hesabu 24:17,19.
Hapa twaona kwamba, Mungu anamfunulia nabii Baalam kwamba Yesu atakapokuja atakuwa “mwenye kutawala”, Yakobo yeye anamwita “mwenye miliki”. Yesu ndiye mtawala na mimliki wa maisha yako na yangu, anahitaji tumpatie umiliki wa mambo yetu yote ili apate kutawala. Yeye mwenyewe akiwa hapa duniani aliwahi kusema.
“Kaeni ndani Yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa matunda lisipokaa ndani ya mzabibu, vivyo hivyo ninyi msipokaa ndani Yangu hamwezi kuzaa matunda. Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani Yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana, maana pasipo Mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lo lote.” Yohana 15:1-4. “Ye yote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu.” Mathayo 10:37
Nabii Isaya alieleza kuwa Yesu ni Nani?
Nabii Isaya aliitwa kuhudumu kama nabii miaka 600 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu. Mungu alimpatia ufunuo nabii Isaya juu ya kuja kwa Yesu aitwaye Masihi akisema
“Kwa maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume, nao utawala utakuwa mabegani mwake. Naye ataitwa: Mshauri wa Ajabu, Mungu Mwenye Nguvu, Baba wa Milele, Mfalme wa Amani.” Isaya 9:6
Katika aya hii tunaambiwa na nabii wa Mwenyezi Mungu, nabii Isaya kwamba, Yesu ni “Mfalme wa Amani, Baba wa Milele na Mungu mwenye Nguvu”
Uhusiano wako na Yesu utategemea sana ufahamu huu ambao tunaangalia katika maandiko. Iwapo utampokea Yesu kama nabii wa kawaida, sawa na Manabii wengine, utashindwa kuona thamani yake katika maisha yako ya sasa na hata ya milele. Lakini kama utampokea kama jinsi alivyofunuliwa na mababii wa Mwenyezi Mungu, utakuwa umefikia kilele cha kusudi la Mungu la kumtuma Yesu kuja hapa duniani. Yesu ni zaidi ya nabii. Katika aya hizi tulizoangalia tumeona kwamba Yeye Yesu ni, Mfalme aliyetarajiwa muda mwingi na manabii wa kale, na tena ni Mungu mwenye nguvu.
Nabii Isaya anaelezeaje tena kuhusu Yesu, Je Yesu ni nani tena?
Pamoja na sifa hizi za kuwa mfalme, matawala na Mwenye enzi. Mungu alimpatia ufunuo tena nabii Isaya akieleza juu ya kazi ambayo Yesu angekuja kuifanya atakapokuwa hapa duniani. Katika kitabu cha Isaya 53 :4-9.
“Hakika alichukua udhaifu wetu na akajitwika huzuni zetu,…Lakini alitobolewa kwa ajili ya makosa yetu, alichuburiwa kwa maovu yetu, adhabu iliyotuletea sisi amani ilikuwa juu yake, na kwa majeraha yake sisi tumepona. Sisi sote, kama kondoo, tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe, naye BWANA aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa na kuteswa, hata hivyo hakufungua kinywa chake, aliongozwa kama mwana kondoo apelekwaye machinjoni, kama vile kondoo anyamazavyo mbele ya amkataye manyoya, hivyo hakufungua kinywa chake. Kwa kukamatwa na hukumu aliondolewa… Kwa maana alikatiliwa mbali na nchi ya walio hai, alipigwa kwa ajili ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na waovu, pamoja na matajiri katika kifo chake, ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. 10Lakini yalikuwa ni mapenzi ya BWANA kumchubua na kumsababisha ateseke, ingawa BWANA amefanya maisha yake kuwa sadaka ya hatia”.
Zamani kabisa kabla hata Yesu hajazaliwa, miaka 600 kabla, Mungu aliwafunulia manabii kwamba Yesu angekuja kufa msalabani kama sadaka ya fidia ya makosa yetu. Kwamba BWANA angeweka juu ya Yesu maovu yetu sisi. Hivyo kwa mujibu wa Ufunuo wa Mwenyezi Mungu kwa nabii Isaya, Yesu ni Mwokozi wetu. Ndiyo maana “kwa majeraha yake sisi tumepona”.
Kwamba Yesu ni Mwokozi wa ulimwengu huu, yeye mwenyewe alitangazwa na Malaika Gablieli akisema “kwa maana yeye ndiye atakaye waokoa watu wake kutoka katika dhambi zao” Mathayo 1:21. Rafiki yangu itakuwa ni jambo la kushangaza iwapo tutayakataa hata maneno ya Malaika wa Mungu ambaye inaaminika ndiye ambaye huleta ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa manabii. Hii itamaanisha kwamba, kama tutatilia mashaka maneno haya ya malaika wa Mwenyezi Mungu, hatutaamini kitabu cha Mwenyezi Mungu chochote kile.
Yesu mwenyewe aliwahi kujishuhudia akisema “Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele” Yohana 10:10 “Mimi ni nuru ya ulimwengu Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima” Yohana 8:12. Kisha Yesu anahitimisha kwa kusema kwamba ikiwa watu hawatamwamini kuwa Yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu huu, basi watakufa katika dhambi zao, bi maana hawataweza kuokolewa. Tunasoma haya katika Yohana 8:24.
“Kwa maana msipoamini ya kwamba mimi Ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”
Pia katika Yohana 3:19 Yesu anasema;
“Ye yote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu.”
Haitoshi kusema unamwamini Yesu, hoja ya msingi ni je unamwamini kama nani? Swali la Yesu kwa wanafunzi wake, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? Bado ni swali kwako na kwangu. Namna tutakavyojibu swali hili huelezea hatima ya maisha yetu ya baadaye, Ama Yesu ni Mfalme wa Wafalme na Bwana wa Mabwana ikiwa ni ishara ya kuukubali ufalme wake wa milele ujao, au ni Mwokozi, ikiwa ni ishara ya kutambua kwamba bila yeye hatuwezi kuifikia pepo ya Mwenyezi Mungu. Tunaambiwa katika maandiko matakatifu kwamba, “wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote. Kwa maana hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”. Matendo 4:12. Pia Twapaswa kumwamini Yesu kama Mwanapekee wa Mungu aliyetumwa na Mungu kuja kuukomboa ulimwengu. Hii itamaanisha kuwa tunampokea Yesu si tu kama manabii wengine bali mwenye cheo cha juu kabisa na aliyetukuka. Mungu aliyefanyika mwili akakaa pamoja nasi ili atuonyeshe njia ya kufanyika watoto wa Mungu.
“Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi takauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli” Yohana 1:14.
Injili ya Bwana Yesu inasema kuwa Yesu ni nani?
Je ni wadhifa gani mwingine ambao Yesu aliutangaza kuwa angeufanya?
Katika kitabu cha Yohana 5:22 Yesu anasema
“Wala Baba hamhukumu mtu ye yote, lakini hukumu yote amempa Mwana, 23ili wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba.”
Zaidi ya kwamba Yesu ni Mfalme, Mwana wa Mungu, Mungu Mwenye nguvu na Mwokozi wetu, hapa Yesu anajitangaza kuwa yeye ndiye hakimu atakayeuhukumu ulimwengu huu.
Mtume Muhammad (s.a.w) alitabiri kuwa nabii Isa (Yesu) atakuja kuuhukumu ulimwengu huu. Tunasoma katika Sahihi Bukhari
وَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ، لَيُوشِكَنَّ أَنْ يَنْزِلَ فِيكُمُ ابْنُ مَرْيَمَ حَكَمًا عَدْلاً
“Kwake yeye ambaye nafsi yangu i mikononi mwake, hakika hivi karibuni atashuka kwenu mwana wa Maryamu (Nabii Isa) kama hakimu mwadilifu...” (Sahihi Bukhari hadith namba 3448)
Mandhari ya hukumu hiyo alifunuliwa nabii wa Mwenyezi Mungu Daniel kama tulivyoona hapo juu akisema
“Nikatazama, hata viti vya enzi vikawekwa…maelfu elfu wakamtimikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa…Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Daniel 7:13-14.
Rafiki yangu mpendwa ni kwamba, Yesu amekabidhiwa hukumu yote. Sababu ya Yesu kupewa hukumu mwenyewe aliieleza kwamba, “Naye amempa Mwanawe mamlaka ya kuhukumu kwa kuwa Yeye ni Mwana wa Adamu” Yohana 5:27. Maandiko matakatifu mara kwa mara yameweka wazi jambo hili kuwa dunia itahukumiwa na Yesu atakapodhihirishwa kwa kurudi kwake mara ya pili. “Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu uliwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua kwake huyo, amewahakikishia watu wote kwa kumfufua Yeye kutoka kwa wafu” Matendo 17:31.
Hivyo basi ingekuwa heri kiasi gani kama tutasimama upande wa hakimu huyu. Kusimama upande wake kutamaanisha kuepuka hukumu. Yesu amewahakikishia wamwaminio kwamba hawataingia hukumuni akisema “Ye yote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu”. Yohana 3:18.
Yesu akiwa hapa duniani aliwahi kuelezea mandhali ya hukumu hii itakavyokuwa. Katika Mathayo 25:31-46 anasema
“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. Mataifa yote watakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi. Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wake wa kushoto. Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’ Ndipo wale wenye haki watakapomjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha au ukiwa na kiu tukakunywesha? Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au ukiwa uchi tukakuvika? Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’ “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlimvyotendea mmojawapo wa hawa ndugu Zangu walio wadogo, mlinitendea Mimi.’ Kisha atawaambia wale walio upande Wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele alioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’ Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi , au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’ Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’ Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele”.
Kisa hiki cha jinsi Yesu atakavyotoa hukumu siku ili ya mwisho kimeelezwa pia kwa usahihi wake katika Sahihi Muslim Kitabu 32 Hadith Namba 6232;
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ز إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَقُولُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: يَا ابْنَ آدَمَ، مَرِضْتُ فَلَمْ تَعُدْنِي. قَالَ: يَا رَبِّ كَيْفَ أَعُودُكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ؟ قَالَ: أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ عَبْدِي فُلَانًا مَرِضَ فَلَمْ تَعُدْهُ؟ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّكَ لَوْ عُدْتَهُ لَوَجَدْتَنِي عِنْدَهُ. يَا ابْنَ آدَمَ: اسْتَطْعَمْتُكَ فَلَمْ تُطْعِمْنِي، قَالَ: يَا رَبِّ وَكَيْفَ أُطْعِمُكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ؟ قَالَ: أَمَا عَلِمْتَ أَنَّهُ اسْتَطْعَمَكَ عَبْدِي فُلَانٌ فَلَمْ تُطْعِمْهُ؟ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّكَ لَوْ أَطْعَمْتَهُ لَوَجَدْتَ ذَلِكَ عِنْدِي. يَا ابْنَ آدَمَ: اسْتَسْقَيْتُكَ فَلَمْ تَسْقِنِي، قَالَ: يَا رَبِّ كَيْفَ أَسْقِيكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ؟ قَالَ اسْتَسْقَاكَ عَبْدِي فُلَانٌ فَلَمْ تَسْقِهِ، أَمَا إِنَّكَ لَوْ سَقَيْتَهُ لَوَجَدْتَ ذَلِكَ عِنْدِي
Amesimulia Abu Huraira (r.a), “Amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) Hakika Mwenyezi Mungu S.W atasema siku ya kiyama. Ee mwanadamu, nilikuwa mgonjwa lakini hukuja kuniona. Atasema: Ee Bwana wangu, nitawezaje kukutembelea ikiwa wewe ni Bwana wa ulimwengu? Allah atasema, je hukujua kwamba mja wangu huyu na yule alikuwa mgonjwa lakini hukuenda kumtembelea? Na je hukulifahamu hili kwamba kama ungemtembelea ungenikuta mimi kwake? Ee mwanadamu, nilikuomba chakula lakini hukunilisha. Naye atasema, Bwana wangu nitawezaje kukulisha hali wewe ni Bwana wa ulimwengu? Atasema Mwenyezi Mungu, Je hukujua kwamba mja wangu huyu na yule alikuomba chakula lakini hukumlisha? Je hukufahamu kwamba, kama ungemlisha ungenikuta mimi kando yake? Allah atasema tena, Eee mwanadamu, nilikuomba maji lakini hukunipa. Naye atasema, Eee Bwana wangu ningewezaje kukupa wewe maji nawe ni Bwana wa ulimwengu? Allah atasema, mja wangu huyu na yule alikuomba maji lakini, na kama ungemnywesha maji, ungenikuta mimi karibu yake
Zingatia kuwa Yesu katika kitabu cha Mathayo 25:31 anasema kwamba atakuja na Malaika. Na atakuwa ameketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake. Tukio hili la kuja kwa Yesu katika utukufu wake litaashiria mwisho wa dunia na kwamba kiayama kitakuwa kimetukaribia. Wakati huo tunaambiwa na vitabu vitakatifu kwamba Mbingu zitakunjwa kama karatasi. Katika kitabu cha Ufunuo 6:14 twasoma;
“mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa vikahamishwa kutoka mahali pake…watajificha katika pango na chini ya miamba ya milima wakiiambia milima ‘tuangukieni, tusitirini mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi…”
Pia Quran inakubaliana na maneno haya ya kwamba mbingu zitakunjwa kama karatasi
Sura ya 21:104 tunasoma;
يَوْمَ نَطْوِي السَّمَاءَ كَطَيِّ السِّجِلِّ لِلْكُتُبِ كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ وَعْدًا عَلَيْنَا إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ
“Siku tutakayoikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi…”
Iwapo mbingu zitakunjwa kama karatasi ni hakika kwamba tukio hili lazima liwe ni tukio la mwisho wa dunia na siku ya kiyama.
Qurani inakubaliana na swala hili la watu kukusanywa siku ya kiyama na kuhukumiwa. Katika Sura ya 4:87 tunasoma;
اللَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ لَيَجْمَعَنَّكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللَّهِ حَدِيثًا
“Mwenyezi Mungu hakuna anayestahiki kuabudiwa ila yeye tu, kwa yakini Atakukusanyeni siku ya kiama…”
Quran Sura ya 84:1. Fafanuzi ya Tafsir ya ibin Abas (Tanwir al-miqibas min tafsir ibin Abas) tunaambiwa kwamba mbingu zitapasuka na Bwana atakuja na Malaika zake na katika aya ya 4 tunasoma kuwa “ardhi itawatoa waliomo makaburini”
Quran Sura ya 2:210 pia tunaambiwa;
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن يَأْتِيَهُمُ اللَّهُ فِي ظُلَلٍ مِّنَ الْغَمَامِ وَالْمَلَائِكَةُ وَقُضِيَ الْأَمْرُ وَإِلَى اللَّهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ
“Hawangojei ila Mwenyezi Mungu awafikie katika vivuli vya mawingu na Malaika, au hukumu iwe imekwisha tolewa, na kwa Mwenyezi Mungu hurejezwa mambo yote”
Quran Sura ya 89:22 tunaambiwa kwamba Malaika hawa watakuwa wamemzunguka Bwana “safu safu” atakapokuwa akija
وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا
“Na akaja Mola wako Mlezi na Malaika safu safu, “
Katika Quran Yesu ametajwa kuwa ni dariri ya kiama. Sura ya 43:61 Tunasoma;
وَإِنَّهُ لَعِلْمٌ لِّلسَّاعَةِ فَلَا تَمْتَرُنَّ بِهَا وَاتَّبِعُونِ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ
“Na kwa kweli (yeye Nabii Isa) ni alama ya Kiyama (kuwa kinaanza kutukaribia): msikikifanyie shakea…”.
Katika Kitabu cha Ufunuo 22:12 Yesu anasema
“Tazama naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo”
Maneno haya ya Yesu yanapatikana pia katika Quran Sura ya 39:70
وَوُفِّيَتْ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُوَ أَعْلَمُ بِمَا يَفْعَلُونَ
“Na kila nafsi itapewa sawa sawa yale iliyoyafanya, naye anajua sana wanayoyatenda.”
Kumbe kuja kwa Yesu ni alama ya hukumu kwamba imekwisha kufika. Na yeye ndiye atakayehukumu ulimwengu huu na kulipa watu kutokana na matendo yao atakapokuja. Hatakuja peke yake, bali vitabu vyote vinasema atakuja na wingu kubwa la Malaika wa Mbinguni. Ni hakika iliyoje kwamba Yesu siyo tu Nabii wa kawaida kama manabii wengine, bali ni wa pekee na kustahili heshima kubwa kama tutakavyoona hapo baadaye. Uelewa wako na wangu juu ya hili ni muhimu sana ili tuweze kumpatia Yesu hadhi yake kama vitabu vinavyotufunulia. Kumfahamu namna hii kutaathiri pia namna tunavyohusiana naye. Ndiyo maana Yesu siku zote atakuwa na swali hili kwako “Je wewe unaniita mimi kuwa nani?”
Sifa nyingine za Yesu ndani ya Vitabu vitakatifu ni zipi?
Yesu ni Muumbaji.
Tunaposoma katika Injili ya Bwana Yesu katika kitabu cha Yohana Sura 1:-3 Tunaambiwa maneno haya
Hapo mwanzo, alikuwako Neno. Huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu. Vitu vyote viliumbwa kwa Yeye, wala pasipo Yeye hakuna cho chote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa…Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu Wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli.
Hapa anatajwa “Neno” kuwa alikuwa pamoja na Mungu, kwa njia ya huyu Neno kila kitu katika ulimwengu huu kiliumbwa. Kisha baadaye inamalizia kwa kusema, huyu Neno ndiye aliyefanyika mwili akakaa pamoja nasi. Hapa tunahitaji kumfahamu huyu aitwaye Neno la Mungu ni nani?
Katika Quran 3:45 tunaambiwa kwamba Yesu ni neno
إِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّهَ يُبَشِّرُكِ بِكَلِمَةٍ مِّنْهُ اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ
”(Kumbukeni) Malaika waliposema: Ewe Mariam! Hakika Mwenyezi Mungu anakupa khabari njema za neno litokalo kwake, jina lake ni Masihi Isa Mwana wa Mariam…”
Ikiwa Yesu ndiye Neno, basi ni kweli pia kwa mujibu wa Yohana 1:14 kwamba Yeye Yesu ndiye huyo aliyefanyika mwili kwa kuzaliwa hapa na tukauona utukufu wake. Hivyo basi kuzaliwa kwake hapa duniani hakukuwa ndiyo mwanzo wake, bali kama maandiko yasemavyo, alikuwepo milele zote na kwa yeye vitu vyote vilifanyika. Wakolosai 1:16-17 tunasoma kwamba;
“Kwa Yeye vitu vyote vilivyoko mbinguni na juu ya nchi viliumbwa, vile vitu vinavyoonekana na vile visivyoonekana, kama ni viti vya enzi au falme, au wenye mamlaka au watawala, vitu vyote viliumbwa na Yeye na kwa ajili Yake. Yeye alikuwapo kabla ya vitu vyote na katika Yeye vitu vyote vinashikamana pamoja.”
Dhana hii ya uweza wa Yesu wa kuumba inakubalika pia ndani ya Quran. Yesu anatangaza uwezo huu wa kuumba katika Sura ya 3:49
ز...أَنِّي قَدْ جِئْتُكُم بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ .أَنِّي أَخْلُقُ لَكُم مِّنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ فَأَنفُخُ فِيهِ فَيَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِ اللَّهِ وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّهِ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَس
“… Hakika mimi nimewajilieni na dalili itokayo kwa Mola wenu. Mimi nitakufanyieni katika udongo kama namna ya ndege, kisha nampulizia ndani yake (awe) ni ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu…”.
Yesu akiwa hapa duniani kwa mujibu wa Qurani aliendelea kuwa na uwezo huo wa kuumba kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu tumeona katika Yohana 1:1-3 kwamba Yeye siku zote alikuwa na Mungu walifanya kazi kwa pamoja katika kuumba dunia hii, ndiyo maana bado aliendelea kuumba kwa idhini hiyo hiyo aliyopewa tokea mwanzo. Hakuna nabii anayeweza kupewa heshima hii ya uumbaji isipokuwa yuna namna ya Mungu. Mwenyezi Mungu mwenyewe amesema katika kitabu cha Isaya 42:8
“Mimi ndimi BWANA, hilo ndilo jina langu! Sitampa mwingine utukufu wangu”.
Sifa ya uumbaji ndiyo inayomtofautisha Mungu na miungu ya uongo na sanamu na vitu vingine vilivyoumbwa. Hawezi kumpatia mtu mwingine hivi hivi. Yeye aliumba wanadamu kutokana na udongo na kuwapulizia pumzi ya uhai. Ndivyo Yesu pia alivyofanya, aliumba ndege kutokana na udongo na akawapulizia pumzi wakawa hai na kuruka. Tunapokiri sifa hii ya uumbaji ya Yesu ni lazima tutamtofautisha na manabii wa kawaida. Sifa za Yesu ni sifa dhahiri zinazotokana na matendo yake na wala siyo sifa za kutangaziwa na wanadamu na kufanywa kile asivyo Yeye. Wapo manabii wengi wa uongo siku hizi wanajipatia sifa lukuki wao wenyewe ama kupewa na wafuasi wao sifa za mdomoni tuu na kupewa majina makubwa makubwa hali matendo yao hayaonyeshi sifa hizo, Yesu ni zaidi ya manabii.
Yesu ni Mponyaji.
Hubiri la kwanza la Yesu baada ya kutoka kufunga siku 40 jangwani linatangaza sifa ya uponyaji ya Yesu. Katika Luka 14:18-19 Yesu anatangaza huduma yake kwa kusema;
“Roho wa Bwana yu juu Yangu, kwa sababu amenitia mafuta kuwaletea maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaweka huru wanaoonewa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika”
Qur’an nayo pia inakubaliana na ukweli huu kwamba Yesu alitiwa nguvu kwa Roho Mtakatifu. Sura ya 2:87 tunasoma kwamba;
ز...وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ أَفَكُلَّمَا جَاءَكُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنفُسُكُمُ اسْتَكْبَرْتُمْ فَفَرِيقًا كَذَّبْتُمْ وَفَرِيقًا تَقْتُلُونَس
“…na tukampa Isa mwana wa Mariam miujiza mingi na tukampa nguvu kwa roho Takatifu…”
Qur’an hapa inatueleza kwamba Yesu alipewa miujiza mingi. Miujiza hii ni kama ilivyotangazwa na Yesu mwenyewe katika Luka 4:18-19. Katika Quran Sura ya 5:110 tunaona baadhi ya miujiza hii aliyopewa Yesu ni kuponya watu.
إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ اذْكُرْ نِعْمَتِي عَلَيْكَ وَعَلَىٰ وَالِدَتِكَ إِذْ أَيَّدتُّكَ بِرُوحِ الْقُدُسِ تُكَلِّمُ النَّاسَ فِي الْمَهْدِ وَكَهْلًا وَإِذْ عَلَّمْتُكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَالتَّوْرَاةَ وَالْإِنجِيلَ .وَإِذْ تَخْلُقُ مِنَ الطِّينِ كَهَيْئَةِ الطَّيْرِ بِإِذْنِي فَتَنفُخُ فِيهَا فَتَكُونُ طَيْرًا بِإِذْنِي .وَتُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ بِإِذْنِي .وَإِذْ تُخْرِجُ الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِي .وَإِذْ كَفَفْتُ بَنِي إِسْرَائِيلَ عَنكَ إِذْ جِئْتَهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ
“(Kumbuka) Mwenyezi Mungu atakaposema: Ewe Isa bin Mariam! Kumbuka neema yangu juu yako, na ujuu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utu uzima. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipotengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, na ulipowaponyesha, vipofu na wakoma kwa idhini yangu, na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu…”
Rafiki yangu msomaji nataka nikuhakikishie kwamba Yesu ni Mponyaji na anao uwezo wa kukuponya hata leo. Vitabu vyote vitakatifu vinashuhudia kwamba Yesu huyu yuko hai mbinguni hata sasa. Hivyo bado akingali na uwezo wa miujiza hiyo mingi aliyopewa kuifanya. Na bila shaka muujiza wa uponyaji haujakoma bado. Kama utamuomba ataweza kusikia shida yako na kuiponya.
Yesu ni Mfalme na Bwana wa Mabwana
Katika Biblia Wafilipi 2:9 tunasoma kwamba;
“Kwa hiyo tena, Mungu alimwadhimisha mno. Akamkirimia jina lile lipitalo kila jina. Ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA…”
Rafiki yangu angalia hapa kwamba Mungu anataka kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA. Mini na wewe tunatakiwa kutambua hili, ili Yesu anapukuuliza sasa hivyi ya ya kwamba “wewe wa nena ya kuwa mimi ni nani?” jibu liwe kwamba wewe ndiwe BWANA.
Qur’an pia inakubaliana na dhana hii ya kutukuza kwa Yesu na kwamba kila goti la vitu vya mbinguni (bi maana Malaika) na vitu vya duniani (bi maana wanadamu) lipigwe kwake. Sura ya 3:45 tunasoma kwamba;
”(Kumbukeni) Malaika waliposema: Ewe Mariam! Hakika Mwenyezi Mungu anakupa khabari njema za neno litokalo kwake, jina lake ni Masihi Isa Mwana wa Mariam, Mwenye heshima ulimwenguni na Akhera na ni miongoni mwa wenye kukurubishwa (mbele za Mwenyezi Mungu).
Yesu anatakiwa kuheshimiwa hapa duniani na mbinguni pia. Yeye mwenyewe alipokuwa hapa duniani aliwahi kusema hili. Katika Mathayo 28:18 tunasoma kwamba;
“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani..”
Ndiyo maana Quran nayo ilipokuja ilifunua kuwa Yesu ana “heshima ulimwenguni na Akhera”.
Rafiki yangu, kama nilivyotangulia kusema hapo mwanzo. Ibilisi anatambua kwamba iwapo watu watamfahamu Yesu kama alivyodhihirishwa katika maandiko matakatifu, basi watapata uzima wa milele. Hivyo anajitahidi kutumia kila njia kuinua watu makundi makundi wakileta mafundisho yasiyo sahihi ili kuwapotoa watu katika ukweli huu. Hii ndiyo maana Yesu aliyaita chachu ya mafarisayo. Baada ya kusoma maandiko haya bila shaka umegundua kwamba Yesu ni zaidi ya nabii wa kawaida, kinyume kabisa na jinsi ulivyofundishwa hapo awali. Na sasa pamoja nami unataka kujibu kwa usahihi swali la Yesu ambalo linakujia mara kwa mara likiuliza “Je wewe wanena kuwa Yesu ni nani?” Na sasa ni kusudi lako kujibu. Yesu ni Bwana, ni Mwokozi, ni Mponyaji, ni hakimu anayekuja kuhukumu dunia hii na ni Mfalme wa Wafalme mwenye heshima duniani na mbinguni. Na kwamba atakuja hivi karibuni kama mhukumu wa ulimwengu huu. Nawe ni kusudi lako kuepukana na hukumu hii kwa kumchagua kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako. Usisite kufanya hivyo. Ungana na wale wengine walioamua kumpatia Yesu maisha yao ili awe kiongozi wao. Pia endelea kusoma vitabu vingine vyenye ujumbe huu ili uweze kufahamu zaidi, na Mwenyezi Mungu akubariki sana.