Mwenyezi Mungu ametoa mwongozo ambao kwa kuufuata huo mwanadamu ataweza kumjua Mungu wa kweli, kuepukana na uovu na hatimaye kuishi maisha ya milele ng’ambo ya kaburi. Mwongozo huo unapatikana kupitia vitabu vyake vitakatifu. Vitabu hivi, yaani, Qur’an tukufu na Biblia Takatifu, vyote vinanadi ya kwamba ni mwongozo kwa watu wa Mungu.
Qur’an inasema katika suratul Baqara 2:2 kwamba;
ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ
“Hiki ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu.”
Kadhalika, Biblia pia katika 2Timotheo 3:16-17 inasema kwamba;
“Kila andiko lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”
Ikiwa vitabu vya Mwenyezi Mungu ndiyo huo mwongozo wetu ili tuweze kumfahamu Mungu na kuwa wacha Mungu tukitenda mema, basi ni vizuri sana tuweze kuwa na elimu ya kutosha juu ya vitabu hivi vitakatifu.
Kwa mujibu wa Qur’an tukufu, Mwenyezi Mungu aliteremsha vitabu gani?
Tunasoma katika Qur’an kwamba;
إِنَّآ أَنزَلْنَا ٱلتَّوْرَىٰةَ فِيهَا هُدًۭى وَنُورٌۭ ۚ يَحْكُمُ بِهَا ٱلنَّبِيُّونَ ٱلَّذِينَ أَسْلَمُوا۟ لِلَّذِينَ هَادُوا۟ وَٱلرَّبَّـٰنِيُّونَ وَٱلْأَحْبَارُ بِمَا ٱسْتُحْفِظُوا۟ مِن كِتَـٰبِ ٱللَّهِ وَكَانُوا۟ عَلَيْهِ شُهَدَآءَ ۚ فَلَا تَخْشَوُا۟ ٱلنَّاسَ وَٱخْشَوْنِ وَلَا تَشْتَرُوا۟ بِـَٔايَـٰتِى ثَمَنًۭا قَلِيلًۭا ۚ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْكَـٰفِرُونَ
“Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu na nuru; ambayo kwayo Manabii walio nyeyekea, na wacha Mungu na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu (hicho) cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni mimi. Wala msibadilishe aya zangu kwa thamani chache. Na wasiohukumu kwa aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndiyo makafiri” (Suratul Maida 5:44).
Aya hii inasema kwamba, kwanza Mwenyezi Mungu aliteremsha Taurati, na kwamba Taurati hiyo ina uongofu na nuru, na Taurati hiyo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu. Taurati hii alipewa Nabii Musa.
Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu ni vitabu gani vingine ambavyo Mwenyezi Mungu aliviteremsha kabla ya Qur’an?
وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِمَن فِى ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ ۗ وَلَقَدْ فَضَّلْنَا بَعْضَ ٱلنَّبِيِّـۧنَ عَلَىٰ بَعْضٍۢ ۖ وَءَاتَيْنَا دَاوُۥدَ زَبُورًۭا
“Na Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine, na Daudi tulimpa Zaburi” (Suratul Israa 17:55).
وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِى ٱلزَّبُورِ مِنۢ بَعْدِ ٱلذِّكْرِ أَنَّ ٱلْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِىَ ٱلصَّـٰلِحُونَ
“Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema” (Suratul Anbiyaa 21:105).
Qur’an inaeleza kwamba pamoja na Taurati Mwenyezi Mungu pia alishusha Zaburi kwa Nabii Daudi, ambayo ndani yake kuna ahadi nzuri ya kwamba nchi ambayo Mwenyezi Mungu anaiandaa (yaani, Pepo ya Mwenyezi Mungu) waja wema ndiyo watakaoirithi. Hii ni ahadi nzuri sana, kwamba Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake kiasi kwamba amewaandalia nchi nzuri watakapo kaa milele zote. Itakuwa vyema kumtii Mungu kiasi kwamba atuingize katika nchi hiyo. Mimi ninatamani kuiona nchi hiyo, na bila shaka na wewe msomaji ni miongoni mwa wenye tamanio hili.
Je ni Kitabu gani kingine Mwenyezi Mungu aliteremsha baada ya Taurati na Zaburi?
وَقَفَّيْنَا عَلَىٰٓ ءَاثَـٰرِهِم بِعِيسَى ٱبْنِ مَرْيَمَ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلتَّوْرَىٰةِ ۖ وَءَاتَيْنَـٰهُ ٱلْإِنجِيلَ فِيهِ هُدًۭى وَنُورٌۭ وَمُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلتَّوْرَىٰةِ وَهُدًۭى وَمَوْعِظَةًۭ لِّلْمُتَّقِينَ
“Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na Nuru na inayosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wacha Mungu” (Suratul Maida 5:46).
Aya hii inasema kwamba, baada ya Torati na Zaburi, Mwenyezi Mungu aliteremsha Injili kupitia Isa bin Maryam. Qur’an inaweka wazi kwamba katika Injili mna uongofu na Nuru na pia ni mawaidha kwa wacha Mungu.
Mpaka hapa tunaona kwamba Mwenyezi Mungu kabla ya Qur’an tukufu, aliteremsha Taurati, Zaburi, na Injili. Vitabu hivi vyote, Qur’an inasema vina sifa zifuatazo;
1. Ni Nuru 2. Ni uongofu kwa wacha Mungu, na 3. Ni Mawaidha mema.
Je kuna uwezekano kwamba vitabu hivi vya Mwenyezi Mungu vimechafuliwa na watu na sasa haviaminiki tena?
وَكَيْفَ يُحَكِّمُونَكَ وَعِندَهُمُ ٱلتَّوْرَىٰةُ فِيهَا حُكْمُ ٱللَّهِ ثُمَّ يَتَوَلَّوْنَ مِنۢ بَعْدِ ذَٰلِكَ ۚ وَمَآ أُو۟لَـٰٓئِكَ بِٱلْمُؤْمِنِينَ
“Na huwaje wakufanye wewe hakimu nao wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanageuka. Na hao si wenye kuamini” (Suratul Maida 5:43).
وَلْيَحْكُمْ أَهْلُ ٱلْإِنجِيلِ بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فِيهِ ۚ وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ فَأُو۟لَـٰٓئِكَ هُمُ ٱلْفَـٰسِقُونَ
“Na wahukumu watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu” (Suratul Maida 5:47).
Aya hizi Mbili zinaonyesha kwamba, hadi Mtume Muhammad (s.a.w) alipokuja bado Wayahudi na Wakristo walikua na Taurati, Zaburi na Injili zilizokuwa na hukumu za Mwenyezi Mungu ndani yake. Na kwa vitabu hivyo walitakiwa kuwahukumu watu. La sivyo, Mwenyezi Mungu asingeamrisha kwamba watu wa Injili wanatakiwa kuhukumu kwa yale yaliyo ndani yake ikiwa vitabu hivyo vingekuwa vimeharibiwa. Kwa kweli hakuna mahali popote katika Qur’an Tukufu ambapo inasema kwamba vitabu hivyo, Taurati na Injili, vimeharibiwa au kutiwa mikono.
Je vipi kuhusu Suratul Maida 5:48, mbona yaonekana kama vile Qurani inasema Taurati na Injili vimeharibiwa?
Ukweli ni kwamba, lipo tatizo la wafasiri wengi wa Qur’an ambao hufasiri kama wapendavyo wao wenyewe na kuongeza maneno yao katika kitabu cha Mwenyezi Mungu ili kuwapotosha watu. Aya hii ukiisoma katika matini ya Kiarabu (Lugha asili ya Qur’an) haisemi maneno ambayo yapo katika tafsiri ya Kiswahili. Hapa tutaleta aya hii katika Tafsiri Mbali mbali za Qur’an.
Tafsiri ya Shekhe Abdallah Salehe Al-Farsy.
وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّۢ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةًۭ وَمِنْهَاجًۭا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًۭا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“Na tumekuteremshia Kitabu kwa (ajili ya kubainisha) haki, kinachosadikisha vitabu vilivyokuwa kabla yake, na kuvihukumia (kama haya ndiyo yaliyoharibiwa au ndiyo yaliyosalimika). Basi wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia. Na kila (umma) katika nyinyi (binadamu) tumejaalia sharia yake na njia yake. Na kama Mwenyezi Mungu angalitaka angekufanyeni kundi moja (la kufuata sharia moja), lakini anataka kukujaribuni kwa hayo aliyokupeni. Basi shindaneni kuyafikilia mambo ya kheri. Nyinyi nyote marudio yenu ni kwa Mwenyezi Mungu, naye atakuambieni (yote) yale mliyokuwa mkikhitilafiana.”
Ikiwa utaisoma aya hii kwa Kiswahili na kudhani kwamba hayo ndiyo maneno ya Mwenyezi Mungu yalivyo, utaishia kudhani kwamba, kusudi la kuteremshwa Qur’an ni kuja kuhukumia au kupima vitabu vilivyotangulia kwamba ni mambo gani katika vitabu hivyo yameharibiwa na mambo gani humu yamesalimika bila kuharibiwa. Hivyo aya hii yaweza kuonekana kama Ushahidi kwamba Qur’an inaeleza kuwa vitabu vya kale vilivyotangulia vimeharibiwa na sasa haviaminiki tena.
Ukweli ni kwamba tunaposoma aya hiyo hiyo katika tafsiri zingine za Qur’an haisemi maneno hayo kwa Kiswahili. Tuangalie baadhi ya Tafasiri hapa.
Tafsiri ya Shekhe Hassani Ali Mwalupa.
وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّۢ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةًۭ وَمِنْهَاجًۭا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًۭا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“Na tumekuteremshia kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia. Na kila (Umma) katika ninyi, tumejaalia sheria yake na njia yake. Na kama Mwenyezi Mungu angalitaka angewafanya umma mmoja, lakini ni kuwajaribu katika hayo aliyowapa. Basi shindaneni katika mambo ya kheri. Marejeo yenu nyote ni kwa Mwenyezi Mungu; Naye atawaambia yale mliyokuwa mkikhitilafiana.”
Shekhe Muhsin Al- Bwarwani
وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّۢ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةًۭ وَمِنْهَاجًۭا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًۭا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate Matamanio yao ukaacha haki iliyo kujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kwamba Mwenyezi Mungu angalitaka angekufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni kukujaribuni kwa aliyokupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyokuwa mkikhitilafiana.”
Tafsiri ya Shekhe Ali Juma Mayunga.
وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّۢ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةًۭ وَمِنْهَاجًۭا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًۭا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“Na tumekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda, basi wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia. Kila mmoja wenu tumemjaalia desturi na njia maalumu, na kama Mwenyezi Mungu angependa angekufanyeni kundi moja, lakini anataka kukujaribuni kwa hayo aliyokupeni. Basi shindaneni katika mambo ya kheri, ninyi nyote marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu. Basi atawaambieni yale mliyokuwa mkikhitilafiana.”
Tafsiri ya Maulana Sheikh Mubarak Ahmad Ahmadi H.A.
وَأَنزَلْنَآ إِلَيْكَ ٱلْكِتَـٰبَ بِٱلْحَقِّ مُصَدِّقًۭا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ ٱلْكِتَـٰبِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَٱحْكُم بَيْنَهُم بِمَآ أَنزَلَ ٱللَّهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَآءَهُمْ عَمَّا جَآءَكَ مِنَ ٱلْحَقِّ ۚ لِكُلٍّۢ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةًۭ وَمِنْهَاجًۭا ۚ وَلَوْ شَآءَ ٱللَّهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةًۭ وَٰحِدَةًۭ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَكُمْ فِى مَآ ءَاتَىٰكُمْ ۖ فَٱسْتَبِقُوا۟ ٱلْخَيْرَٰتِ ۚ إِلَى ٱللَّهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًۭا فَيُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“Na tumekuteremshia kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Kitabu, na kukihifadhi, basi uwahukumu baina yao kwa yale Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia; kila mmoja wenu Tumemjaalia desturi na njia maalumu; na kama Mwenyezi Mungu angalipenda angewafanyeni kundi moja, lakini anataka kuwajaribu kwa hayo aliyowapeni. Basi shindaneni katika mambo ya kheri. Ninyi nyote marudio yenu ni kwa Mwenyezi Mungu, naye atawaambieni yale mliyokuwa mkikhitilafiana.”
Tumeangalia Tafsiri za Qur’an zipatazo tano juu ya aya hiyo (Suratul Maida 5:48) na katika tafsiri hizo ni moja tu ile iliyoandikwa na Shekhe Abdalla Salehe Al-Farsy peke yake ndiyo inasema kwamba Qur’an imekuja kuhukumia vitabu kuona kama haya ndiyo yameharibiwa na haya ndiyo yamesalimika. Katika aya hiyo, kuna maneno mengi ambayo Shekhe Farsy ameyaweka ya kwake mwenyewe kando ya Maneno ya Qur’an. Hii ndiyo Tafsiri inayosomwa na Waislamu wengi wanaozungumza lugha ya Kiswahili, na kwa aya hii wengi wamehitimisha kwamba vitabu vilivyoteremshwa kabla ya Qur’an, (Taurati, Zaburi na Injili) yaonekana kwamba vimeharibiwa na wanadamu. Hii si kweli, kwani tumeona mashekhe 4 wote wanapingana na Farsy katika tafsiri zao, na wote wanne wako sawa sawa hawapingani kwa tafsiri zao. Huenda unaweza kusema kwamba mashekhe hawa wamekubaliana katika tafsiri hiyo kwa kuwa wanaitikadi moja (dhehebu) na itikadi hiyo inapingana na shekhe Farsy, hapana. Hebu tuwaangalie mashekhe hawa itikadi zao.
Shekhe Abdallah Salehe Al-Farsy: Yeni ni Mwislamu wa madhehebu ya Suni.
Shehe Muhsini Barwani: Naye pia ni Mwislam wa madhehebu ya Suni.
Shekhe Hasani Ali Mwalupa: Yeye ni Mwislamu wa dhehebu la Shia.
Shekhe Ali Juma Mayunga: Mwislamu wa dhehebu la Shia.
Shekhe Sheikh Mubarak Ahmad Ahmadi H.A: Yeye ni Mwislamu wa dhehebu la Ahmadiyya.
Unaweza kuona kwamba hawa mashekhe ni wa itikadi mbali mbali, lakini wote wanakubaliana juu ya tafsiri ya aya hiyo. Tuangalie ukweli wa aya hii.
Neno مُهَيْمِنًا ambalo Abdallah Farsy analitafasiri kama kuhukumia (kisha akaongeza maneno “kama haya ndiyo yameharibiwa na haya ndiyo yaliyosalimika”) Mashekhe wote wamelitafasiri kama kulinda au kuhifadhi. Hivyo badala ya kusema kwamba Qur’an imekuja kuhukumia vitabu vilivyopita (Taurati, Zaburi na Injili) badala yake ukweli ni kwamba Qur’an imekuja kulinda vitabu hivyo. Kwa hiyo basi, kwa mujibu wa aya hii, Qur’an ni mlinzi wa vitabu vya kale ili visiharibiwe. Kwa maana nyingine ni kwamba hadi Qur’an inashuka, vitabu hivi vilikuwa sahihi, na kwa kuwa sasa Qur’an ipo, itaendelea kuvilinda vitabu hivi.
Je ni kwa vipi Qur’an ni mlinzi wa vitabu vya kale (Taurati, Zaburi na Injili)?
Wengi leo wanatilia mashaka iwapo Vitabu vya Kale ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Visa vingi vya Biblia mfano, Uumbaji wa Mwenyezi Mungu, kisa cha Nuhu na gharika, kisa cha Yona kukaa katika tumbo la samaki kwa siku tatu, kisa cha wana wa Israeli kupita katika bahari iliyopasuka na nchi kavu ikaonekana, na vingine ndani ya Biblia, vyote vimerudiwa tena katika Qur’an, na hivyo kuthibitishia kwamba maneno hayo ni sahihi na yameendelea kuwepo pia ndani ya Qur’an tukufu.
Je ni kwa nini leo Wengi hawaamini kama vitabu vya kale (Taurati, Zaburi na Injili) vingali sahihi?
Katika siku za hivi karibuni kumejitokeza watu wanaojiita “waalimu” na wahubiri wa dini ambao huzunguka huku na huku wakihubiri kwenye mikutano na makongamano mbali mbali. Watu hawa wanahubiri wakinadi kwamba vitabu vya kale vimetiwa mikono ama kuharibiwa na watu, kwa hiyo wanawashawishi watu wasiviamini vitabu hivyo. Wanafanya hivyo kwa kupindua tafasiri za Biblia Takatifu katika baadhi ya aya. Tuangalie baadhi ya madai ya walimu hawa.
Ikiwa Mwenyezi Mungu aliteremsha vitabu vya Taurati, Zaburi na Injili, je kitabu cha Biblia kilitoka wapi?
Wengi wa wale wanaowaongoza watu kutilia mashaka vitabu vya kale wanahoji swali hili ili kuonyesha ushahidi kwamba ni kweli vitabu hivi havipo, vimebadilishwa na watu wameandika kitabu kingine kinachoitwa Biblia ambacho Mwenyezi Mungu hakuwahi kukiteremsha.
Madai haya yanatokana na kukosa kufahamu mambo muhumu yahusuyo maandiko matakatifu. Ukweli ni kwamba, kwa mujibu wa Qur’n Mwenyezi Mungu hakuishia kuteremsha vitabu vinne tu, kwa mfano Qur’an inasema;
إِنَّ هَـٰذَا لَفِى ٱلصُّحُفِ ٱلْأُولَىٰصُحُفِ إِبْرَٰهِيمَ وَمُوسَىٰ
“Hakika haya yamo katika vitabu vya mwanzo, Vitabu vya Ibrahimu na Musa.” (Suratul Al-Aa’la 87:18-19)
Kutokana na aya hii kwa mujibu wa Qur’an tukufu, kuna vitabu vingine zaidi ya Taurati, Zaburi na Injili, hapa tunaona kitabu kingine ni kitabu cha Ibrahimu. Qur’an pia inasema.
وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِى ٱلزَّبُورِ مِنۢ بَعْدِ ٱلذِّكْرِ أَنَّ ٱلْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِىَ ٱلصَّـٰلِحُونَ
“Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.” (Suratul Anbiyaa 21:105)
Pamoja na vitabu vya Ibrahimu, Taurati, Zaburi, Injili, kuna kitabu kingine kinaitwa Kumbukumbu. Hivyo basi tunahitaji kuwa na uelewa sahihi juu ya vitabu ambavyo Mwenyezi Mungu aliteremsha kwa manabii wake. Kwa kutokana na Ushahidi huu Mwenyezi Mungu alishusha vitabu vingi zaidi ya hivyo vinne ambavyo wanachuoni wa Kiislamu wanafundisha watu.
Kitabu Kiitwacho Biblia.
Neno Biblia siyo neno la Kiswahili sipokuwa limetoholewa kutoka neno la Kiyunani Biblos lenye maana ya mkusanyiko wa vitabu. Kwa maana hii, Biblia siyo kitabu kimoja, ni mkusanyiko wa vitabu vingi ambavyo Mwenyezi Mungu aliwashushia manabii. Vitabu vinavyojulikana na Waislamu wengi ambavyo Mwenyezi Mungu alishusha ni vitabu vinne tu, yaani Taurati, Zaburi, Injili na Qur’an. Lakini tunaposoma Qur’an inasema kwamba;
وَرُسُلًۭا قَدْ قَصَصْنَـٰهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًۭا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ ۚ وَكَلَّمَ ٱللَّهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًۭ
“Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno.” (An-Nisaa 4:164).
Kutokana na aya hii, Muhammad hakufunuliwa habari za baadhi ya Mitume na Manabii wa Mwenyezi Mungu na Vitabu ambavyo aliwateremshia mitume hao. Manabii hao wa Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Qur’an wanatokana na kizazi cha wana wa Israeli.
وَوَهَبْنَا لَهُۥٓ إِسْحَـٰقَ وَيَعْقُوبَ وَجَعَلْنَا فِى ذُرِّيَّتِهِ ٱلنُّبُوَّةَ وَٱلْكِتَـٰبَ وَءَاتَيْنَـٰهُ أَجْرَهُۥ فِى ٱلدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُۥ فِى ٱلْـَٔاخِرَةِ لَمِنَ ٱلصَّـٰلِحِينَ
“Na tulimtunukia Ibrahimu Is-haq na Yaaqub. Na tukajaalia katika dhulia zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.” (Suratul AnNaam 6:84)
Tunaona kwamba kumbe Mwenyezi Mungu aliwajaalia wana wa Israel kuwa na manabii wenye kupewa kitabu. Hivyo basi, ni sahihi kusema kwamba, kwa wana wa Israeli Mwenyezi Mungu alishusha vitabu vingi zaidi hivyo vya Taurati, Zaburi na Injili. Katika Biblia kuna vitabu jumla ya 66 ambavyo viliandikwa na manabi (watu wa Mungu) wapatao 40 katika kipindi cha miaka takribani 40. Hivyo Biblia ina mkusanyiko wa vitabu hivyo vya manabii wa wana wa Israeli ambao Mwenyzi Mungu aliwavuvia.
Je katika Yeremia sura ya 8:8 mbona Biblia yenyewe yaonekana kutangaza kwamba kalamu ya waandishi imefanya Torati kuwa ya uongo?
Wahubiri wengi wa dini ya Kiislamu huitumia aya hii kuashiria kwamba Taurati imebadilishwa na waandishi. Usomaji wa makini wa aya hii unaonyesha kinyume cha madai hayo. Tuiangalie kwa makini aya hii.
“Mwasemaje, Sisi tunayo akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya Waandishi imeifanya kuwa uongo” (Yeremia 8:8).
Hapa ni Neno la Mwenyezi Mungu kupitia kinywa cha Nabii Yeremia kwa wayahudi ambao waliridhika kusema kwamba wanayo Torati pamoja nao, lakini hawaifuati. Sababu iliyowafanya wasiifuate Torati ni kutokana na waalimu wa Torati hiyo. Kipindi hicho kulikuwa na watu waliitwa waandishi. Hawa waandishi waliandika vitabu vingine vingi vya kuifafanua Torati kwa watu. Ni katika kufafanua kwao huko ndiko ambako kulipotoa maana ya Torati na hivyo ikaonekana uongo, siyo kwamba Torati iliharibiwa. Mfano halisi ni hapo juu ambapo tumeona wafasili mbali mbali wa Qur’an juu ya sura ya 5:48. Mmoja wao ameongeza maneno yake ambayo hayapo kwenye Qur’an, ingawa kufanya hivyo hakuibadili Qur’an, inabaki kama ilivyo katika matini yake. Kupotoa kwake tafsiri kumefanya Qur’an iseme yale ambayo haisemi. Aya ya 9 ya Yeremia 8 inafafanua vizuri hoja hii.
“Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana wana akili gani ndani yao?”
Yeremia anasema watu wamelikataa neno la Bwana wakafuata yale ambayo kalamu ya waandishi inawalekeza. Hii ni sawa na neno la Mungu lililonenwa kupitia Nabii Isaya akisema;
“Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa huni karibia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa…” (Isaya 29:13).
Mwenyezi Mungu amewapatia wanadamu mwongozo wake ambao wanapaswa kuufuata, kufanya hivyo litakuwa jambo jema kwetu sote. Ndiyo maana Bwana Yesu naye aliwahi kusema kwamba;
“Mwayachunguza Maandiko, kwa sababu mnadhani ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia” (Yohana 5:39).
Yesu anasema kwamba Usomaji wa Maandiko matakatifu unatupatia uzima wa milele, ndiyo maana yanaitwa mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu. Yesu anaendelea kusema kwamba;
“…Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu” (Mathayo 22:29).
Kumbe kutosoma maandiko matakatifu kunaweza kutufanya tupotee. Hii ni kwa sababu, kutosoma maandiko kutatufanya kuupoteza mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu. Bila kuwa na mwongozo huu tutapotea. Hii ina maana kwamba, ikiwa kuna watu siku hizi wanatufundisha kuvikataa vitabu vitakatifu vya Mwenyezi Mungu vikiwemo Taurati, Zaburi, Injili na vitabu vya manabii wengine kama vilivyo kusanywa katika Biblia, basi mtu huyo anataka kutukosesha Mwongozo kwa wamchao Mwenyezi Mungu, na mwisho wa wakati, tutapotea.
Rafiki yangu mpendwa usikubali kushawishika kuvikataa vitabu vitakatifu, kwa kuwa kufanya hivyo kutakupelekea upetevuni. Anza sasa kujisomea Biblia kwani ndani yake mna uzima wa milele.