Vitabu vitakatifu vyote (Biblia Takatifu na Qur’an Tukufu) vinatutaahadharisha juu ya kiumbe aitwaye Shetani kuwa ndiye adui yetu mkubwa, na kwamba tunapaswa kuchukua tahadhari juu ya kiumbe huyu.
Tangazo la kwanza la Mwenyezi Mungu kwa Adam na Mkewe kule peponi kabla hawajaasi amri ya Mwenyezi Mungu lilikuwa ni kuwatahadharisha juu ya adui yao mkubwa, yaani Shetani.
“Enyi watu kule vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhaahiri” (Sura ya 2:168).
“Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo. Basi asikutoeni katika Bustani hii, mkaingia mashakani” (Taha:117).
“Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Motoni” (Faatir :6).
Mwenyezi Mungu anasema Shetani ni Adui yetu dhahiri.
Kazi nyingine ya Shetani imeelezwa katika Qur’an kwamba;
“Waambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shetani, huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shetani ni Adui aliye dhahiri kwa mwanadamu” (Sura ya 17:53).
Hivyo ni wazi kwamba ikiwa kuna ugomvi baina ya ndugu na ndugu ni kwa sababu, Shetani ndiye anaye wachonganisha. Ikiwa kuna vita baina ya taifa na taifa ni kwa sababu, Shetani anayachonganisha mataifa hayo kupigana. Ikiwa kuna ugomvi katika familia kati ya baba na mama, ni kwa sababu Shetani analeta fitina hiyo baina yao.
Biblia pia inaweka wazi kwamba Shetani au Ibilisi ni adui yetu mkubwa kwa kusema;
“Mwe na kiasi na kukesha kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye huzunguka zunguka, akitafuta mtu ammeze” (1Petro 5:8).
Yeye Shetani ni mwongo na baba wa uongo na muuaji.
“Yeye alikuwa mwuuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo” (Yohana 8:44).
Hivyo tunaona, si tu kwamba Shetani analeta uogmvi na uadui baina yetu, lakini pia yeye ni chanzo ya matatizo yote yaliyopo juu ya uso wa dunia. Mauaji, ukatili wa aina zote, magonjwa ya kutisha na mambo mabaya mengine.
Lakini pia, Shetani ni adui wa Mwenyezi Mungu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu ameumba nyota na vimondo kwa ajili ya kumponda Shetani;
“Na kwa hakika tumeipamba mbingu ya karibu kwa mataa, na tumeyafanya ili kuwapiga mashetani, na tumewaandalia adhabu ya Moto uwakao kwa nguvu.” (Al-Muluk 67: 5).
Je Mwenyezi Mungu alimuumba Shetani, ili kuja kufanya uadui na wanadamu?
Baada ya kuona jinsi vitabu vya Mwenyezi Mungu vinavyotutahadharisha dhidi ya Shetani, swali la kujiuliza litakuwa, sasa huyu Shetani alitoka wapi hasa? Je, kwa nini mwenyezi Mwenyezi Mungu atuumbie kiumbe huyu ambaye ni adui yetu mkuu? Tunavigeukia tena vitabu vitakatibu (Biblia Takatifu na Qur’an Tukufu) kuona huyu Shetani alitoka wapi hasa.
Biblia katika Ezekiel 28:13-15 inaeleza kisa cha anguko la Malaika mkuu aliyekuwa katika Bustani ya Mungu kwamba;
“Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa Kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku uliyoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (Ezekieli 28:13-15).
Katika aya hizi kuna kiumbe anayetajwa mwenye sifa ambazo tunahitaji kuzifafanua kwa kina ili tuweze kuwa na uelewa ni kiumbe wa namna gani anayezungumzwa hapa. Tuangalie tafasiri za kamusi mbali mbali juu ya neno Kerubi.
Kerubi: Malaika mwenye mabawa aliyeelezewa katika utamaduni wa kibiblia kama mhudumu wa Mungu…na anayeonekana katika Malaika wa jadi ya Kikristo kama Malaika wa daraja la pili…” Mshiriki wa daraja la pili la Malaika. Makerubi waliowekwa na Mungu kwenye mlango wa paradiso (Mwanzo 3:24) walikuwa Malaika walioumbwa siku ya tatu, na kwa hiyo hawakuwa na umbo dhahiri; mara nyingine huonekana kama wanaume au wanawake, au kama roho au viumbe vya kimalaika. Ni kiumbe mwenye mabawa aliyetajwa zaidi ya mara 90 katika Biblia akihudumu mbele za Mungu, baadaye, anaonekana kama daraja la pili la Malaika.
Hivyo, kwa Maelezo haya ya kamusi mbali mbali za Biblia ikiwemo na kamusi ya Kiyahudi tunagundua kwamba, Kerubi ni aina ya Malaika. Malaika wapo wa aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na aina nyingine ya Malaika waitwao Maserafi. “Hakuna mashaka kwamba Makerubi wa Kibiblia ni aina ya Malaika…Wanaonekana mahali pote (ndani ya Biblia) wakiwa katika uwepo wa Mungu na katika kumtumikia Yeye” (The SDA Bible Commentary Vol. 8).
Kerubi afunikaye: Katika Biblia tunasoma kitabu cha Kutoka 25:8 kwamba, Mwenyezi Mungu alipomwita Musa katika mlima wa Sinai, alimpatia maagizo mengi ikiwemo kazi ya kujenga hema ya kukutania (Patakatifu) ambapo Bwana angekutana na watu wake. Mungu anamwambia Musa kwamba; “Nao na wanifanyie patakatifu ili nipate kukaa kati yao, sawasawa na haya ninayokuonyesha” (Kutoka 25:8). Hii inamaanisha kwamba, hema hiyo ya kukutania ilijengwa “sawasawa” na yale ambayo Musa alikuwa akionyeshwa, kwa maana ya yale ya Mbinguni; katika “hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake isiyo ya ulimwengu huu” (Waebrania 9:11). Katika kitabu cha Kutoka sura ya 25:19-20 Musa anaambiwa maneno haya;
“Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema na nyuso zao zitaelekeana, hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema”.
Ikiwa Musa alikuwa anajenga hema yenye mfano wa hema ya mbinguni isiyojengwa kwa mikono ya mwanadamu, hii inaonyesha kwamba, hema hii iliyojengwa na Musa ilikuwa mfano, yenye taswira ya ile ya mbinguni, na kwa maana hiyo, kiti cha rehema hicho kiliwakilisha kiti cha enzi mbinguni. Hivyo basi ni sahihi kusema kwamba makerubi hao walikifunika kiti cha enzi kwa mabawa yao. Hivyo katika kitabu cha Ezekieli 28:13 inaposema kerubi afunikaye, inamaana kwamba Malaika huyu alikuwa akikifunika kiti cha enzi cha Mungu.
Tunapoangalia katika Kitabu cha Mwanzo 3:24, Biblia inasema kwamba, Bwana Mungu “akaweka Makerubi upande wa Mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima”. Hii inaonyesha kwamba, pamoja na kazi zingine ambazo Makerubi hawa hufanya pia waliwekwa kuilinda bustani ya Edeni.
Biblia inasema kwamba Malaika huyu alikwa ndani ya Adeni, Bustani ya Mungu, na kwamba katika bustani hiyo aliwekwa akawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu. Ni nini maana ya kuwa juu ya mlima mtakatifu? Na huo mlima mtakatifu wa Mungu ni nini hasa?
Mlima mtakatifu wa Mungu: Neno Mlima wa Bwana limetumika mara nyingi katika Biblia Takatifu, na ili kuelewa maana yake itabidi tuchunguze aya chache za Biblia kwa namna ambavyo neno hili limetumiwa, kwa mfano;
“Na itakuwa kataika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa juu ya mlima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, njooni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu” (Isaya 2:2-3; Mika 4:1-2).
Aya hizi zinaonyesha kwamba Mlima wa Bwana ni watu wake au Kanisa lake (Mlimani kwa Bwana, Nyumbani kwa Mungu wa Yakobo).
Tumeona hapo juu kwamba, Mungu alikuwa amemwambia Musa afanye “Patakatifu”, na kwamba kupitia patakatifu hapo, Mungu angekaa katikati yao. Kisha Mungu kupitia kinywa cha mtumishi wake Daudi anasema, “lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo…” (2Nyakati 6:6). Hivyo nyumbani mwa Bwana, yaani katika Hekalu lake takatifu, ndiyo mlima wake mtakatifu.
Wazo hili linawekwa wazi vizuri, tunaposoma katika kitabu cha Zaburi 24:3 kwamba, “Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakaye sismama katika patakatifu pake? Hivyo ni wazi kwamba, Mlima mtakatifu wa Bwana, ni makao yake, hekaluni mwake.
Sasa Biblia inatuambia kwamba, huyu Kerubi afunikaye (Malaika anayefunika kiti cha enzi cha Mungu), aliwekwa kuwa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, ikimaanisha kwamba, yeye alikuwa juu ya malaika mbinguni (katika mlima wa nyumba ya Mungu). Yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa malaika wengine huko mbinguni, na pia katika Adeni, bustani ya Mungu.
Dhana hii inapatikana pia ndani ya mafundisho ya dini ya Kiislamu tunapochunguza vitabu vya wanachuoni wakubwa wa Kiislamu. Tuwaangalie wanachoni, Imamu Twabariy katika Tarekhe Twabariy juzuu ya 1 uk.
حدثنا القاسم بن الحسن، قال: حدثنا الحسين بْنُ دَاوُدَ، قَالَ: حَدَّثَنِي حَجَّاجٌ، عَنِ ابْنِ جُرَيْجٍ، قَالَ: قَالَ ابْنُ عَبَّاسٍ: كَانَ إِبْلِيسُ مِنْ أَشْرَافِ الْمَلائِكَةِ وَأَكْرَمِهِمْ قَبِيلَةً، وَكَانَ خَازِنًا عَلَى الْجِنَانِ، وَكَانَ لَهُ سُلْطَانُ سَمَاءِ الدُّنْيَا، وَكَانَ لَهُ سُلْطَانُ الأَرْضِ.
“Imesimuliwa na Qaasimu bin Al-Hasan, amesema: amesimulia Husein bin Dauda, amesema: amenisimulia Hajjaaju, kutoka kwa ibn Juraij, amesema: amesema ibn Abaas: Ibilisi alikuwa miongoni mwa kabila la malaika wakuu na wenye kutukuka ambao walikuwa walinzi wa bustani (pepo—Janna), yeye alikuwa sulutani wa mbingu za dunia…”
حَدَّثَنَا ابْنُ حُمَيْدٍ، قَالَ: حَدَّثَنَا سَلَمَةُ بْنُ الْفَضْلِ، عَنِ ابْنِ إِسْحَاقَ، عَنْ خَلادِ بْنِ عَطَاءٍ، عَنْ طَاوُسٍ، عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، قَا كَانَ إِبْلِيسُ قَبْلَ أَنْ يَرْكَبَ الْمَعْصِيَةَ مِنَ الْمَلائِكَةِ اسْمُهُ عَزَازِيلُ، وَكَانَ مِنْ سُكَّانِ الأَرْضِ، وَكَانَ مِنْ أَشَدِّ الْمَلائِكَةِ اجْتِهَادًا، وَأَكْثَرِهِمْ عِلْمًا،
“Imesimuliwa na ibn Humaydi amesema: imesimuliwa na Salamat bin Al-Fadhwli, kutoka kwa ibn Ishaaq, kutoka kwa Khaalidi bin A’twaai, kutoka kwa Twaus, kutoka ibn Abbasi, amesema, Kabla Ibilisi hajaasi alikuwa miongoni mwa Malaika, jina lake alikua Azazeli, na alikuwa…miongoni mwa mwalaika mwenye nguvu na elimu nyingi…”
حَدَّثَنَا مُوسَى بْنُ هَارُونَ الْهَمْدَانِيُّ، قال: حدثنا عمرو بن حماد، قال: حدثنا أسباط، عن السدي، في خبر ذكره عن أبي مالك وعن أبي صالح، عن ابن عباس- وعن مرة الهمداني عن ابن مسعود- وعن ناس من اصحاب النبي ص، قال: لَمَّا فَرَغَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ مِنْ خَلْقِ مَا أَحَبَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ، فَجَعَلَ إِبْلِيسَ عَلَى مُلْكِ سَمَاءِ الدُّنْيَا وَكَانَ مِنْ قَبِيلَةٍ مِنَ الْمَلائِكَةِ يُقَالُ لَهُمُ الْجِنُّ، وَإِنَّمَا سُمُّوا الْجِنَّ لأَنَّهُمْ خُزَّانُ الْجَنَّةِ، وَكَانَ إِبْلِيسُ مَعَ مُلْكِهِ خَازِنًا،
“Imesimuliwa na Musa bin Haaruna Al-Hamdaniy, amesema: Imesimuliwa na Amru bin Hamaad, amesema: Imesimuliwa na Asbatwi, kutoka kwa Al-Sadiy katika khabari iliyotajwa Abiy Maaliki na kutoka ibn Swaalih, kutoka kwa ibn Abaas na kutoka kwa Al-Hamdaniy kutoka ibn Masuud na kutoka kwa Swahaba wa Mtume (s.a.w), amesema: zama Mwenyezi Mungu alipomaliza kuumba kama alivyopenda yeye, alistarehe katika arshi, akamjaalia Ibilisi miliki ya mbingu za dunia. Yeye (Ibilisi) alikuwa miongoni mwa kabila la Malaika waliokuwa kwakiitwa Majini. Wao waliitwa majini kwa sababu walikuwa wakilinda pepo (bustani), Ibilisi alikuwa mtawala wa walinzi hao…”
Nukuru hizi kutoka kwa wanachuoni wa Kiislam zinaonyesha kuwafikiana na kile Biblia ilichosema kwamba; kulikuwepo na Malaika mkuu aliyetukuka, kiongozi wa Malaika wengine. Biblia inasema alikua katika Adeni, Bustani ya Mungu, Wanachuoni wa Kiislamu pia wanakubaliana kwamba Ibilisi alikuwa miongoni mwa Malaika waliokuwa wanaitwa Majini. Malaika hawa waliitwa majini kwa sababu wao walikuwa walinzi wa peponi, (pepo kwa kiarabu inaitwa Jannat). Hivyo Jinni maana yake ni Mlinzi wa pepo (au bustani). Kumbuka pia Biblia inasema kwamba, Adamu na Eva walipoasi Mungu aliwafukuza kutoka katika Bustani ya Edeni, na akaweka Makerubi (Malaika kama tulivyoona hapo juu) kuilinda njia ya Bustani.
Kutoka Malaika mkuu hadi kuwa Shetani
Mpaka sasa tumeona kuwa, alikuwepo Malaika mkuu, ambaye alikuwa kiongozi wa Malaika wengine. Biblia inasema alikuwa Kerubi afunikaye na alikuwa katika bustani ya Adeni. Vitabu vya wanachuoni wa Kiislamu vinasema alikuwa mtawala wa walinzi wa bustani (Jannat) na kwamba walinzi hao waliitwa majini. Katika sehemu hii tutaangalia ni kwa namna gani sasa aligeuka na kuwa shetani?
Kitabu cha Ezekieli kinaendelea kusema kwamba,
“Ulikuwa mkamilifu katika njia zako, tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako” (Ezekieli 28:15).
Tunaona kwamba kumbe “uovu ulionekana” ndani ya huyu kiumbe kwa yeye mwenyewe. Sasa ni uovu gani huo? Illi kugundua kuwa ni uovu gani huo ulioonekana ndani yake tuchunguze Biblia zaidi.
“Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu kuliko nyota za Mungu; nami nitaketi juu ya mlima wa makutano, katika pande za mwisho za kaskazini, nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye aliye juu” (Isaya 14:12-14).
Hivyo, kutokana na aya hii inaonyesha kwamba, ndani ya moyo wa kiumbe huyu malaika mkuu, kulitokea tamaa ya kutaka kufanana na yeye aliye juu, yaani Mwenyezi Mungu. Kitabu cha Ezekieli kinasema uovu ulionekana ndani yake. Yaani kwa tamaa na kiburi cha uzuri wake, kiumbe huyu akashawishika moyoni mwake kujitukuza na kutaka kuabudiwa kama Mungu, anasema nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti change kuliko nyota za Mungu. Ufunuo 1:20 inasema nyota ni Malaika wa Mungu. Hivyo kiumbe huyu mtukufu alitaka kuwa juu ya Mwenyezi Mungu na kuabudiwa na Malaika wengine.
Biblia pia inatuambia kwamba kwa sababu ya uovu huo;
“Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako, umeiharibu hekima kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini…” (Ezekieli 28:7).
Yaonekana kwamba Malaika huyu alikuwa na mwangaza mkubwa na kwa sababu ya mwangaza huo ulimsababisha akawa na kiburi. Katika Isaya 14:12 limetumika neno “, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi “, Neno hili kwa ki Latini ni Lusifa. Hili ni jina lingine la Malaika huyu aliyekuwa na utukufu wa ajabu.
Tuangalie tena Qur’an na vitabu vya wanachuoni kuona jambo hili linaafikiana na mafundisho ya dini ya kiislamu?
حَدَّثَنَا مُوسَى بْنُ هَارُونَ الْهَمْدَانِيُّ، قال: حدثنا عمرو بن حماد، قال: حدثنا أسباط، عن السدي، في خبر ذكره عن أبي مالك وعن أبي صالح، عن ابن عباس- وعن مرة الهمداني عن ابن مسعود- وعن ناس من اصحاب النبي ص، قال: لَمَّا فَرَغَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ مِنْ خَلْقِ مَا أَحَبَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ، فَجَعَلَ إِبْلِيسَ عَلَى مُلْكِ سَمَاءِ الدُّنْيَا وَكَانَ مِنْ قَبِيلَةٍ مِنَ الْمَلائِكَةِ يُقَالُ لَهُمُ الْجِنُّ، وَإِنَّمَا سُمُّوا الْجِنَّ لأَنَّهُمْ خُزَّانُ الْجَنَّةِ، وَكَانَ إِبْلِيسُ مَعَ مُلْكِهِ خَازِنًا، فَوَقَعَ فِي صَدْرِهِ كِبْرٌ، وَقَالَ: مَا أَعْطَانِي اللَّهُ هَذَا إِلا لِمَزِيَّةٍ، هَكَذَا حَدَّثَنِي مُوسَى بْنُ هَارُونَ
“Imesimuliwa na Musa bin Haaruna Al-Hamdaniy, amesema: Imesimuliwa na Amru bin Hamaad, amesema: Imesimuliwa na Asbatwi, kutoka kwa Al-Sadiy katika khabari iliyotajwa Abiy Maaliki na kutoka ibn Swaalih, kutoka kwa ibn Abaas na kutoka kwa Al-Hamdaniy kutoka ibn Masuud na kutoka kwa Swahaba wa Mtume (s.a.w), amesema: zama Mwenyezi Mungu alipomaliza kuumba kama alivyopenda yeye, alistarehe katika arshi, akamjaalia Ibilisi miliki ya mbingu za dunia. Yeye (Ibilisi) alikuwa miongoni mwa kabila la Malaika waliokuwa kwakiitwa Majini. Wao waliitwa majini kwa sababu walikuwa wakilinda pepo (bustani), Ibilisi alikuwa mtawala wa walinzi hao…kukatokea ndani ya kifua chake Kiburi na akasema, Mwenyezi Mungu hakunipatia haya isipokuwa kwa ajili ya uzuri wa utukufu wangu”.
Twabariy anasema kwamba kwa sababu ya uzuri wake Malaika huyu kulitokea kiburi na majivuno moyoni (kifuani) mwake. Sawa-sawa na jinsi tulivyoona Biblia ikisema. Tuendelea kuangalia jinsi kiburi hiki kilivyopelekea Malaika huyu kujaa kiburi na kudai kuwa sawa na Mungu. Katika Qur’an sura ya 21:29 tunasoma,
“Na yeyote kati yao atakayesema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu”
Tafsiri ya Imamu Twabariy juu ya aya hiyo inasema kwamba;”
حَدَّثَنَا القاسم، قال: حدثنا الحسين، قال: حدثني حجاج، عن ابن جريج: «وَمَنْ يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلهٌ مِنْ دُونِهِ» قال: قال، ابن جريج
من يقل من الملائكة إني إله من دونه، فلم يقله إلا إبليس، دعا إلى عباده نفسه، فنزلت هذه الآية في إبليس.
“Imesimuliwa na Qaasimu, amesema: amesimulia Al-Husein, amesema: amesimulia Hajaaj kutoka kwa ibn Juraij {{Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake,}} amesema: amesema ibn Juraij yeyote Miongoni mwa Malaika atakayesema mimi ni mungu badala yake, hakuwahi kusema haya isipokuwa Ibilisi, yeye alidai kuabudiwa mwenyewe aya hii ilishuka kwa ajili ya Ibilisi”.
حَدَّثَنَا بِشْرُ بْنُ مُعَاذٍ، قَالَ: حَدَّثَنَا يَزِيدُ، قال: حدثنا سعيد، عن قتادة: «وَمَنْ يَقُلْ مِنْهُمْ إِنِّي إِلهٌ مِنْ دُونِهِ فَذلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ كَذلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ» ، وإنما كانت هذه الآية خاصة لعدو الله إبليس لما قال ما قال، لعنه الله وجعله رجيما، فقال: «فَذلِكَ نَجْزِيهِ جَهَنَّمَ كَذلِكَ نَجْزِي الظَّالِمِينَ» .
“Amesimulia Bishru bin Mua’dhi: Amesema: amehadithia Yaziid amesema: amesimulia Sai’d kutoka kwa Qataad: {{“Na yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu”}} Aya hii hasa Mwenyezi Mungu anamjibu Ibilisi pale aliposema yale aliyoyasema, Mwenyezi Mungu akamlaani…akasema {{Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu}}”.
Vitabu vyote vinaafikiana kwamba, Malaika (Lusifa) huyo aliyeasi huko mbinguni (peponi) alianza kwanza kuwa na kiburi cha uzuri wake, na kisha ndani yake kukatokea uovu ambao uovu huo ulikuwa ni kutaka kufanana na Mwenyezi Mungu, yaani kudai ibada ambayo ni stahili ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Matokeo ya Uasi
Ufunuo 12:7-9 inasema kwamba;
“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake, nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye”.
Kitendo cha Lusifa kujifananisha na Mungu, kilikuwa ni ishara ya kuleta mapinduzi ufalme wa Mwenyezi Mungu huko mbinguni. Mwenyzi Mungu asingekubaliana na jambo hilo, hii ilipelekea Lusifa kufukuzwa huko mbinguni. Kuna jambo linaanza kujitokeza hapa katika aya hizi, mpaka hapa tumekwisha kuona kwamba, Malaika mtukufu sana aliyeitwa Lusifa ndiye ambaye alijaa kiburi na hatimaye uovu ukaonekana moyoni mwake, sasa hawa malaika aliotupwa pamoja nao walitoka wapi? Tuangalie Biblia na Qur’an zaidi.
Katika kitabu cha Ufunuo 12:3-4 inasema kwamba;
“Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi…”
Kwa mujibu wa Ufunuo 1:20, Nyota ni Malaika, na tayari tumeona katika Ufunuo 12:9 joka ni Shetani au Ibilisi. Hivyo hii inaonyesha kwamba, Lusifa alipoasi huko mbinguni alianza kuwashawishi malaika wa mbinguni ili kuwaingiza katika uasi, akafanikiwa kuwashawishu theluthi moja ya Malaika. Hii ni idadi kubwa sana kwani malaika hawajulikani idadi yao. Danieli aliwahi kupata ufunuo na kuona mandhari ya mbinguni, kuhusu idadi ya malaika alisema;
“…maelfu elfu na elfu kumi mara elfu kumi” Daniel 7:10 (hii ni sawa na 1000 x 1000 x 10,000 x 10,000). Hii ni idadi isiyo hesabika. Halafu ndipo fikiria kwamba Shetani alishawishi theluthi wakawa upande wake. Jeshi la Shetani na malaika wafuasi wake ni kubwa mno, na wote hawa wamefukuzwa mbinguni na kutupwa hapa chini. Biblia inasema;
“…Wala makao yao hayakuonekana tena huko mbinguni” (Ufunuo 12:9).
Qur’an inadokeza juu ya viumbe waliokuwa wakiishi mbinguni na baadaye wakafukuzwa, na kwamba kwa sasa hawaruhusiwi tena kuingia huko. Tunasoma ndani ya Qur’an kwamba;
“Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur’an ya ajabu! Inaongoza kwenye uongofu, kwa hiyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi” (Suratul Jinn 72:1-2).
Hapa tunaona kundi la majini lilisikiliza Qur’an na kuiamini, katika Suratul Ahqaaf 46:29-31 tunapata maelezo ya tukio zima hilo la majini kusikiliza Qur’an, inasomeka kama ifuatavyo:
“Na wakati tulipo waleta kundi la majini kuja kwako kusikiliza Qur’an. Basi walipo ihudhuria walisema: Sikilizeni! Na ilipokwisha somwa, walirudi kwa kaumu yao kwenda kuwaonya. Wakasema: Enyei kaumu yetu! Sisi tumesikia Kitabu kilicho teremshwa baada ya Musa, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake, na kinacho ongoza kwenye Haki na kwenye njia iliyo nyooka. Enyi kaumu yetu! Muitikieni Mwenye kuita kwa Mwenyezi Mungu, na muaminini, Mwenyezi Mungu atakusameheni, na ataku kingeni na adhabu chungu” (Suratul Ahqaaf 46:29-31).
Katika aya hizi tunaona Allah (s.w.t) ndani ya Qur’an kwamba alimpelekea mtume Muhammad (s.a.w) kundi la majini ili wasikilize kisomo cha Qur’an na kwamba walipomaliza kusikiliza wakaamini na kuwa waislam, na sasa wakarudi kwenda kwa majini wenzao kutangaza habari njema walizozisikia kutoka kwa mtume (yaani wakaanza daa’wa au kwa lugha nyingine wakaanza kuwainjilisha wenzao ili nao wawe waislam). Hii inamaana kwamba, hawa majini nao huwalingania majini wenzao na kuwaleta katika uislam. Ikiwa walianza tokea wakati huo, bila shaka mpaka kufikia karne hii watakuwa wameshasilimisha majini wengi sana.
Tumekwisha kuona hapo mwanzo kwamba, unaposema Jinni unamaanisha malaika mwenye cheo cha ulinzi wa Pepo (Bustani ya Mungu), yaani malaika walinzi wa Peponi walijulikana kwa majini. Sasa hebu tuangalie zaidi ndani ya Qur’an ili kubaini majini hawa ni akina nani?
“Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo. Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza, lakini sasa anayetaka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia” (Suratul Jinn 72:8-9).
Kama majini walikuwa ni malaika walinzi wa pepo, basi ni sahihi kusema kwamba, majini ni malaika walioasi kutoka mbinguni na wakafukuzwa wasiingie tena huko, ndiyo maana Biblia ikasema, “na mahali pao hapakuonekana tena huko mbinguni”.
Vitabu vitakatifu vinatukataza kushirikiana na majini kwa njia yoyote ile.
“Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao kizazi baada ya kizazi” (Walawi 17:7).
Biblia hapa inatukataza kufanya ushirika wowote na majini. Hii ni kwa sababu tumeona katika somo hili kwamba, majini ni mashetani walioasi mbinguni, na Mwenyezi Mungu alishawafukuza huko mbinguni, haiwezekani tena sisi tushirikiane nao kwa namna yoyote. Kadhalika pia Biblia inatuambia kwamba:
“Basi mtiini Mungu, mpingeni Shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).
Jambo ambalo watu wa Mungu wanapaswa kulifanya ni kumpinga Shetani kwa nguvu zote. Hata hivyo hatuwezi kumshinda shetani kwa juhudi za kimwili, kwa maana Biblia inatuambia “Maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome” (2Wakorintho 20:4). Mwenyezi Mungu ametupatia maelekezo ya namna ya kumshinda Shetani. Katika kitabu cha ufunuo 12:11 tunasoma:
“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo (Yesu), na kwa neo la Ushuhuda wao; ambao hawakupenda Maisha yao hata kufa” (Ufunuo 12:11).
Njia pekee ya kumshinda Shetani ni kwa kupitia imani katika damu iliyomwagika msalabani, damu ya Yesu, na kwa kupitia neno la ushuhuda, yaani Biblia Takatifu. Shetani anajua sana kwamba imani katika damu ya Yesu (kifo chake katika Msalaba kwa Kalvari) italeta ushindi. Hii ndiyo maana anapambana kuupoteza ukweli huu mioyoni mwa watu. Utasikia huku na huku mafundisho ya “Yesu hakusulubiwa wala kufa msalabani” ikilenga kuhafifisha imani ya watu juu ya kifo cha Yesu katika Msalaba. Lakini pia katika aya hiyo tunaambiwa tutamshinda Shetani kwa neno la ushuhuda, yaani Biblia. Hii nayo shetani anapambana kuhakikisha anahafifisha imani ya watu juu ya Biblia, watatokea waalimu wakijiita waalimu wa dini, nao watawafundisha watu kuwa Biblia haiaminiki tena, imetiwa mikono. Jambo hili ni hatari sana kwa kuwa linatupotezea imani juu ya zana za ushindi dhidi ya Shetani. Mtume Paulo aliandika kwamba:
“Hatimaye, mzidi kuwa Hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” (Waefeso 4:10-12).
Ni wazi kwamba, tuko katika pambano kuu, pambano ambalo lilianzia mbinguni, baina ya Mungu mwenyewe na Shetani na malaika zake. Tupende tusipende tunahusika katika upande mmoja wapo, hivyo kama hatutafahamu ukweli huu tunaweza kujikuta tunapigana kinyume cha Mwenyezi Mungu bila kujua huku tukidhani kwamba tunamtumikia Mwenyezi Mungu.
Rafiki yangu mpendwa ninakusihi fanya uamzi wa kusimama upande wa Mwenyezi Mungu. Katika somo hili tumejifunza historia ya anguko la Shetani huko mbinguni. Tumeona jinsi anavyotumia hila kubwa sana kuwahadaa watu, wakati mwingine atajifanya kuwa ni kiumbe mzuri mwenye kutoa msaada kwa wanadamu kiasi cha kudanganya kuwa amefuata uongofu. Biblia imekwisha kutuonya juu ya hila za Shetani ikisema:
“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru” (2Wakoritho 11;14).Hivyo, haitoshi tu kusema majini wamesilimu, lakini hoja ya msingi itakuwa hao majini ni akina nani na wana msaada gani kwetu? Mafundisho juu ya majini yanayotolewa na mashekhe, je, ni sahihi kiasi gani? Je, majini ndivyo walivyo kama isemavyo Qur’an? Itakuwa jambo la kheri kama ukisimama imara kama Biblia inavyofundisha,
“Basi mtiini Mungu, mpingeni Shetani, naye atawakimbia” (Yakobo 4:7).
Bwana akubariki sana unapoendelea kujifunza. Kwa msaada zaidi unaweza kuwasiliana nasi kupitia ukrasa wa mawasiliano hap katika tovuti hii.