Mnamo Julai 4, 1997 wanaanga wa shirika la NASA nchini Marekani walituma chombo katika sayari ya Mars kilichojulikana kwa jina la Mars Pathfinder, Sojourner rover. Mradi huu uligharimu kiasi cha dola za Kimarekani 265,000,000 sawa sawa na Shilingi za Tanzania, 6,095,000,000,000 (Trilion 6). Kumekuwa na miradi kama hii mingine zaidi ya 5 ambayo kwa jumla imegharimu zaidi ya dola Bilioni 16 (zaidi ya Trilion 368,000). Kwa nini wanaanga hawa wanahangaika kutumia kiasi hiki kikubwa cha pesa wakati ambapo wakazi wengi wa dunia wanakumbwa na baa la njaa, na majanga ya kutisha kama vimbunga, mafuriko, magonjwa ya kutisha nk? Sababu kubwa ni kwamba, wanatafuta sayari nyingine ambayo kuna uwezekano wa kuishi, na huenda ikiwezekana kupata mahali pengine palipo bora zaidi pa mwanadamu kuishi na kufurahia maisha.  Hii ni kwa sababu, kila kunapokucha tunasikia vilio na maombolezo, majanga ya kutisha, vita baina ya taifa na taifa, kabila na kabila, magonjwa ya kutisha, njaa na matetemeko ya nchi, vitendo vya kikatili, dhuluma, ubakaji,  ulawiti na usagaji na kila aina ya uovu juu ya uso wa dunia. Ni sahihi kusema kwamba; “..maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote” (Mwanzo 6:5). Hii imesababisha hofu kutawala juu ya uso wa dunia. Tunaamka leo lakini hatujui kesho yetu itakuwaje. Ndiyo maana Biblia Takatifu ina sema;

“Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia watu wakuu wa dunia wanadhoofika. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele” (Isaya 24:4-5).

Dunia siyo mahali sahihi tena pa kuishi na kufurahia maisha, wanasayansi na watafiti wa mambo ya anga wameanza harakati za kutafuta mahali pengine pazuri pa kuishi ili waihame dunia hii.

Lakini je, kwanini wana sayansi hawa wa anga wahangaike kiasi hicho na kutumia pesa nyingi hivyo? Je Vitabu vitakatifu vinasemaje? Je kuna uwezekano wa kuwa na makao mengine ya mwanadamu yaliyo bora zaidi, ya kupendeza ambapo mwanadamu ataishi akifurahia maisha milele zote? Tuviangalie zaidi vitabu vitakatifu.

Je Qur’an tukufu na hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w) vinafundisha kwamba ipo nchi ambayo watu watafurahia Maisha?

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِى ٱلزَّبُورِ مِنۢ بَعْدِ ٱلذِّكْرِ أَنَّ ٱلْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِىَ ٱلصَّـٰلِحُونَ

“Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema” (Suratul Anbiyaa 21:105).

Aya hii ya Qur’an inasema kwamba Mwenyezi Mungu aliandika katika Zaburi, tuiangalie aya asili katika kitabu cha Zaburi jinsi inavyosema;

“Bali wenye upole, watairithi nchi, watajifurahisha kwa wingi wa amani” (Zaburi 37:11).

“Wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele” (Zaburi 37:22).

Katika Injili ya Bwana Yesu, maneno haya pia yamerudiwa na Yesu mwenyewe katika kitabu cha Mathayo 5:5 ya kwamba;

“Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.”

Je, vitabu vinatupatia maelezo gani ya makao ya milele ya wacha Mungu?

وَٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ ٱلْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ خَـٰلِدِينَ فِيهَا ۚ نِعْمَ أَجْرُ ٱلْعَـٰمِلِينَ

“Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito wakidumu humo. Ni mwema ulioje huo ujira wa watendao mema” (Suratul Ankabut 29:58).

“Na ule mji ni wa mraba, na marefu yake sawasawa na mapana yake. Akaupima mji kwa ule mwanzi; ulikuwa kama maili elfu na mia tano; marefu yake na mapana yake na kwenda juu kwake ni sawasawa. Akaupima ukuta wake, ukapata dhiraa mia na arobaini na nne kwa kipimo cha kibinadamu. Maana yake cha Malaika. Na majenzi ya ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi, mfano wa kioo safi.” (Ufunuo 21:16-18).

“Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwanakondoo, katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa” (Ufunuo 22:1-2).

مَّثَلُ ٱلْجَنَّةِ ٱلَّتِى وُعِدَ ٱلْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ ۖ أُكُلُهَا دَآئِمٌ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى ٱلَّذِينَ ٱتَّقَوا۟ ۖ وَّعُقْبَى ٱلْكَـٰفِرِينَ ٱلنَّارُ

“Mfano wa Bustani waliyoahidiwa wacha Mungu, kati yake inapita mito, matunda yake ni ya daima, na pia kivuli chake. Huu ndiyo mwisho wa wale walio jilinda. Na mwisho wa makafiri ni Moto” (ArRadi 13: 35).

Vitabu vyote, Biblia na Qur’an Tukufu vinaeleza uwepo wa makao ya wacha Mungu, na kwamba katika makao hayo kuna mji wenye maghorofa yaliyojengwa na kupambwa kwa vito vya thamani sana (Tazama pia Ufunuo 21:19-21) ndani yake upo mto na bustani yenye mti wa uzima ndani yake, ambayo majani yake ni ya kuwaponya mataifa. Maelezo haya yaelekea kwamba ni urejeshwaji upya wa Bustani ya Edeni ambayo wazazi wetu  Adamu na Hawa waliipoteza. Ukisoma katika kitabu cha Mwanzo 2:8-10 Biblia inasema;

“Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.”

Kitu pekee ambacho hakionekani kuwepo katika hiyo bustani mpya ni mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Hii ni kwa sababu Mungu atakuwa amekomesha mabaya yote yasiwepo tena.

Ni sahihi basi kusema kwamba hiyo nchi (pepo) ambayo Mungu anawaandalia waja wake inaashiria urejeshwaji upya wa makao yetu ambayo wazazi wetu waliyapoteza. Qur’an inasema;

“…Kama tulivyoanza umbo la mwanzo, tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika sisi ni watendao” (Suratul Anbiyaa 21:104).

Biblia inaafikiana na urejeshwaji upya wa nchi na hivyo kuumbwa kwa bustani ikisema kwamba;

“Waipeleka roho yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi(Zaburi 104:30).

“Naye aketiye juu ya kiti cha enzi akasema, Tazama nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, andika ya kwamba, maneno haya ni amini na kweli” (Ufunuo 21:5).

Hivyo twaona kwamba, licha ya dunia yetu hii kuchakaa na kujawa kila aina ya uovu na dhuluma, Mwenyezi Mungu anatuandalia mbingu mbya na nchi mpya ambamo ndani yake anaweka jiji la wacha Mungu watendao vitendo vyema. Haina haja ya wanasayansi wa anga kuhangaika na kupoteza mapesa mengi kwa ajili ya kutafuta makao bora huko angani, kwani tayari vitabu vitakatifu vinatueleza kwamba, Mwenyezi Mungu mwenyewe anaandaa makao hayo. Yesu alipokuwa hapa duniani akiongea na mwanafunzi wake alisema;

“Msifadhaike mioyoni mwenu, mnamwamini Mungu, niaminini na mimi, nyumbani mwa Baba yangu muna makao mengi, kama sivyo ningaliwaambia, maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili mimi nilipo nanyi muwepo” (Yohana 14:1-3).

Biblia inaweka wazi kwamba, manabii wote wa Mwenyezi Mungu walihubiri na kutarajia mji huu ambao unaandaliwa huko mbinguni.

“Kwa imani [Ibrahimu] alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyokuwa yake, akikaa katika hema, pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye msingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu” (Waebrania 11:9-10).

Tunaambiwa katika Biblia kwamba; “Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni, kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi Bwana wetu Yesu Kristo” (Wafilipi 3:20).

Vitabu vyote Biblia na Qur’an vinatuambia kwamba Yesu (au Nabii Isa) yu hai sasa mbinguni, kwa maana Mwenyezi Mungu alimunyanyua kwake, Qur’an inasema;

بَل رَّفَعَهُ ٱللَّهُ إِلَيْهِ ۚ وَكَانَ ٱللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا

“Bali Mwenyezi Mungu alimuinua Kwake, na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hekima” (Suratul AnNisaa 4:158).

Biblia inawafikiana na Qur’an kwa jambo hili yakwamba;

“Akisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao” (Matendo 1:9).

Huko mbinguni ambako Yesu ameinuliwa, Yeye mwenyewe alieleza kazi anayoifanya huko kama tulivyoona, kuwaandalia mahali, au mji ambapo waja wa Mwenyezi Mungu wataishi milele. Hivyo ikiwa tunatarajia kupata pepo ya Mwenyezi Mungu, ni Nabii Isa (Yesu) ndiye anayeiandaa pepo hiyo na utimilifu wa wakati utakapowadia atakuja kutuchukua kama alivyosema.

Je tunawezaje kuipata pepo hiyo ya Mwenyezi Mungu?

Vitabu vya Mwenyezi Mungu vimeeleza wazi sifa za wale watakaoingia peponi, Qur’an inasema kwamba;

إِلَّا مَن تَابَ وَءَامَنَ وَعَمِلَ صَـٰلِحًا فَأُو۟لَـٰٓئِكَ يَدْخُلُونَ ٱلْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ شَيْـًٔا

“Isipokuwa walio tubu, wakaamini na wakatenda mema. Hao basi wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa chochote.” (Suratul Maryam 19:60).

Hapa tunaona kwamba ili mtu aweze kuingia Peponi, shariti la kwanza ni kuamini (kumwamini Mwenyezi Mungu), Kutubu makosa, au dhambi, na kuendelea kutenda vitendo vyema. Tunaposoma Biblia tunaona ikiafikiana na wazo hili kwamba;

“Yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” (Matendo 16:30-31).

“…Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu” Matendo 2:38.

Vitabu vitakatifu, Biblia na Qur’an tukufu, vyote vinatuelekeza kwamba, ili tuweze kuifikia Pepo ya Mwenyezi Mungu,

  1. Yatupasa kumwamini Mwenyezi Mungu.
  2. Kutubu madhambi yetu.
  3. Kuendelea kutenda matendo Mema.

Hata hivyo siyo rahisi kwa juhudi zetu kuweza kutenda vitendo vyema, hivyo ili kuweza kutenda vitendo vyema, tunapaswa kuwezeshwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, Qur’an inasema kwamba;

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِٱللَّهِ وَٱلْيَوْمِ ٱلْـَٔاخِرِ يُوَآدُّونَ مَنْ حَآدَّ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُۥ وَلَوْ كَانُوٓا۟ ءَابَآءَهُمْ أَوْ أَبْنَآءَهُمْ أَوْ إِخْوَ‌ٰنَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ كَتَبَ فِى قُلُوبِهِمُ ٱلْإِيمَـٰنَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ ۖ وَيُدْخِلُهُمْ جَنَّـٰتٍ تَجْرِى مِن تَحْتِهَا ٱلْأَنْهَـٰرُ خَـٰلِدِينَ فِيهَا ۚ رَضِىَ ٱللَّهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا۟ عَنْهُ ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ حِزْبُ ٱللَّهِ ۚ أَلَآ إِنَّ حِزْبَ ٱللَّهِ هُمُ ٱلْمُفْلِحُونَ

“Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.” (Suratul Mujadilah:22).

Qur’an inaeleza kwa mujibu wa aya hii kwamba; wanaomwamini Mwenyezi Mungu wameandikiwa katika nyoyo zao imani, na kwamba katika kutenda kwao vitendo vyema wanawezeshwa na Roho itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni sawa kabisa na jinsi inavyofundisha Biblia kwamba;

“Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo nayo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu (Waefeso 2:8).  Imani ni kipawa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndiyo maana Qur’an ikasema Mwenyezi Mungu “ameandika katika nyoyo zao imani.”

Biblia inakubaliana na Qur’an kwamba; Roho Mtakatifu wa Mwenyezi Mungu ndiye anaye waongoza watu kutenda vitendo vyema;

“Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na roho wa Kristo, huyo si wake.” (Warumi  8:8-9).

Je ni jambo gani linaweza kutusababisha tukaikosa Pepo ya Mwenyezi Mungu?

Qur’an inaweka wazi kwamba;

إِنَّ ٱلَّذِينَ كَذَّبُوا۟ بِـَٔايَـٰتِنَا وَٱسْتَكْبَرُوا۟ عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَ‌ٰبُ ٱلسَّمَآءِ وَلَا يَدْخُلُونَ ٱلْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ ٱلْجَمَلُ فِى سَمِّ ٱلْخِيَاطِ ۚ وَكَذَ‌ٰلِكَ نَجْزِى ٱلْمُجْرِمِينَ

“Hakika wale wanaozikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu” (Al-Araaf:40).

Qur’an inasema kwamba wale wanaokanusha ishara za Mwenyezi Mungu haiwezekani kuingia Peponi, kwani uwezekano wa wao kuingia Peponi umefananishwa na uwezekano wa ngamia kuingia katika tundu la sindano. Kwa kadri ngamia asivyoweza kuingia katika tundu ya sindano, ndivyo ambavyo yule anayekanusha aya za Mwenyezi Mungu asivyoweza kuingia Peponi. Jambo la msingi ni kufahamu ni aya gani hizo ambazo mtu akizikanusha hataingia peponi. Juu ya aya hizi Qur’an inapozungumzia kuzaliwa kwa Nabii Isa (Yesu) inasema;

قَالَ إِنَّمَآ أَنَا۠ رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَـٰمًا زَكِيًّا  

قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِى غُلَـٰمٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِى بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا

قَالَ كَذَ‌ٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَىَّ هَيِّنٌ ۖ وَلِنَجْعَلَهُۥٓ ءَايَةً لِّلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِّنَّا ۚ وَكَانَ أَمْرًا مَّقْضِيًّا

“(Malaika) akasema: Hakika mimi ni mwenye kutumwa na Mola wako Mlezi ili nikubashirie tunu ya mwana aliye takasika. Akasema, nitampataje mwana hali mwanadamu yeyote hajanigusa, wala mimi si kahaba? (Malaika) akasema: Ndiyo hivyo hivyo Mola wako Mlezi anasema: Haya ni mepesi kwangu! Na ili tumfanye kuwa ni Ishara kwa watu, na Rehema itokayo kwetu, na hilo ni jambo lililo kwisha kuhukumiwa” (Maryam 19:19-21).

Katika aya hii tunaambiwa kwamba, ishara ya Mwenyezi Mungu ni Nabii Isa bin Maryam (au Yesu). Hii inamaanisha kwamba, ikiwa kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu kunaweza kutukosesha Pepo ya Mwenyezi Mungu, kwa maneno mengine ni kwamba, kumkataa Nabii Isa (Yesu), kunasababisha mtu aikose Pepo. Hii ni sawa tunaposoma Biblia inasema kwamba;

“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu, walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo (isipokuwa la Yesu) (Matendo 4:12).

“Amwaminiye Mwana, yuna uzima wa milele, asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhambu ya Mungu inamkalia” (Yohana 3:36).

Yesu Mwenyewe anasema kwamba;

“Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yohana 14:6).

Ni wazi kwamba, vitabu vitakatifu vinatubainishia ya kwamba, iwapo tungependa kuingia Peponi, hakuna njia yoyote ambayo ingetuwezesha isipokuwa ni kupitia Nabii Isa peke yake. Hakuna nabii mwingine ambaye alifanywa kuwa kipatanisho kati yetu na Mwenyezi Mungu. Hata Nabii Muhammad mwenyewe hana daraja hiyo ya kuingiza watu Peponi maana, Allah (s.w.t) alimwambia mtume kwamba;

فَٱعْلَمْ أَنَّهُۥ لَآ إِلَـٰهَ إِلَّا ٱللَّهُ وَٱسْتَغْفِرْ لِذَنۢبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَٱلْمُؤْمِنَـٰتِ ۗ وَٱللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَىٰكُمْ

“Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba aghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa” (Suratul Muhammad 47:19).

Hii ndiyo maana Muhammad hana sifa za kuwaingiza watu peponi, yeye mwenyewe anangojea rehema za Mwenyezi Mungu tu! Lakini tumeona Nabii Isa (Yesu) Mwenyewe ana nadi ndani ya Biblia Takatifu kwamba, mtu hatafika mbinguni (Peponi) isipokuwa kwa njia ya Yesu peke yake. Kwa sababu hiyo ya kuwa na dhambi kama inavyoonyesha Qur’an Tukufu, ndiyo maana Mwenyewe Muhammad anasema kuwaambia waumini wake kwamba;

قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ ٱلرُّسُلِ وَمَآ أَدْرِى مَا يُفْعَلُ بِى وَلَا بِكُمْ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰٓ إِلَىَّ وَمَآ أَنَا۠ إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

“…Mimi si kiroja miongoni mwa Mitume. Wala sijui nitakavyofanywa wala ninyi. Mimi nafuata niliyo funuliwa tu kwa Wahyi, wala mimi si chochote ila ni mwonyaji tu mwenye kudhihirisha wazi” (Suratul Al-Ahqaaf  46:9).

Katika somo hili tumejifunza kwamba; Mwenyezi Mungu amewaandalia waja wake watendao vitendo vyema Pepo ambayo ni makazi ya milele kwa waja hao. Pia tumeona kwamba Nabii Isa, ndiyo yuko mbinguni mpaka sasa, na kazi anayoifanya huko ni kuandaa mahali au Pepo hiyo ambamo ndani yake kuna mji wenye maghorofa watakayokaa hao watakatifu wa Mwenyezi Mungu. Ili kufika huko ni njia moja tu pekee nayo ni kumwamini Nabii Isa kama ishara ya Mwenyezi Mungu na rehema itokayo kwake. Yeye ndiye njia ya kutufikisha huko Peponi.

Rafiki yangu, ni matumaini yangu kwamba utachukua uamzi ulio sahihi ili kuweza kujiponya nafsi yako na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu inayokuja hivi karibuni, wakati Nabii Isa atakapokuja mara ya pili.



Related Information

Imani Je Shetani alitoka wapi? Mwongozo kwa wamchao mwenyezi Mungu Ni nani alimpatia utume Paulo?