إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ. ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“(Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema “Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nikuinue kwangu. Na nikuepushe na wale waliokufuru, na niwafanye wale waliokufata wawe juu ya wale walio kufuru mpaka siku ya Kiyama…” Sulat Maidah 3:55
Baadhi ya watu hawaamini iwapo nabii Isa alikufa na kisha akafufuka kuwa hai na kupandishwa mbinguni. Wengi wa hawa wasioamini kuwa nabii Isa alikufa wanaamini bila shaka yoyote kuwa alipandishwa mbinguni. Lakini tunapoiangalia aya hii ya Qur’an tunagundua kwamba; tukio hili la nabii Isa kupandishwa mbinguni halitokei isipokuwa kwanza limetanguliwa na tukio la kufa. Yaani Mwenyezi Mungu anasema hapa kwamba “Ewe Isa mimi nitakufisha” na ndipo inafuata kauli “na nikuinue” kwa maana ya kwamba, kwanza atamfisha na baadaye atampandisha mbinguni
Ukweli ni kwamba kuna ushahidi mkubwa ndani ya Biblia Takatifu na Qur’an Tukufu unaoonyesha ya kwamba Nabii Isa bin Maryam (a.s) alikufa na kufufuka na kisha akapandishwa mbinguni. Tutaziangalia baadhi ya aya hapa.
1. KAULI YA NABII ISA MWENYEWE NDANI YA QUR’AN TUKUFU.
Surat Maryam 19:33
وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا
“Na amani iko juu yangu siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa kuwa hai”
Hapa kuna tamko la wazi kabisa la Masihi Isa bin Maryam wakati wa kuzaliwa kwake kuwa alitabiri juu ya kifo na ufufuo wake. Ndiyo kawaida ya manabii wa Mwenyezi Mungu kutabiri mambo yajayo.
Kauli hii inawafikiana kabisa na kauli inayopatikana ndani ya Biblia Takatifu katika kitabu cha Mathayo 20:18-19.
Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.
Katika vitabu vitakatifu vyote Biblia na Qur’an tumeona kauli ya wazi ya nabii Isa kutabiri juu ya kufa kwake na kufufuka. Hatutafanya jambo jema kupinga vitabu vya Mwenyezi Mungu, na kwa kweli kufanya hivyo ni kuikana imani, kwani imani ya kweli ni kumwamini Mwenyezi Mungu, Malaika zake, Mitume wake, Vitabu vyake na kuamini siku ya mwisho. Katika Biblia Kitabu cha 2Nyakati 20:20 tunaambiwa pia
Mwaminini Bwana, Mungu wenu ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake ndivyo mtakavyofanikiwa.
Pia tusomapo katika Qur’an, Sulat Maidah (5) aya ya 117 tunaona kauli nyingine aliyoitoa Nabii Isa mbele za Mwenyezi Mungu, baada ya kuwa ameinuliwa hadi mbinguni.
“...وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ. فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ. وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ”
“…Na nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa nao, na uliponifisha, wewe ukawa Mchungaji juu yao, na wewe ni shahidi juu ya kila kitu”
Hakuna shaka yoyote kabisa kuwa nabii Isa alikufa na kufufuliwa kuwa hai kwa mujibu wa Qur’an Tukufu.
Hebu Tuiangalie Sulat Al I’iMlan (3) aya ya 55 tena kwa umakini zaidi.
إِذْ قَالَ اللَّهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ وَمُطَهِّرُكَ مِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَجَاعِلُ الَّذِينَ اتَّبَعُوكَ فَوْقَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ. ثُمَّ إِلَيَّ مَرْجِعُكُمْ فَأَحْكُمُ بَيْنَكُمْ فِيمَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ
“(Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema “Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nikuinue kwangu. Na nikuepushe na wale waliokufuru, na niwafanye wale waliokufata wawe juu ya wale walio kufuru mpaka siku ya Kiyama…”
Aya hii inaonyesha kuwa Nabii Isa aliinuliwa kwa Mungu, maana anasema “nikuinue kwangu” yaani angeinuliwa mpaka kwa Mungu, vilevile kama isemavyo Qur’an katika Sura ya 4:158 kwamba;
بَل رَّفَعَهُ اللَّهُ إِلَيْهِ. وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا
“Bali mweyezi Mungu alimnyanyua kwake….”
Tunapochunguza maandiko matakatifu Biblia, katika kitabu cha Matendo 1:9 inawafiki kabisa dhana hii iliyowekwa ndani ya Qur’an kuwa Nabii Isa angeinuliwa hadi mbinguni;
Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao.
Kuwa Nabii Isa aliinuliwa, ama kupandishwa hadi mbinguni, Biblia na Qur’an vimewafikiana kabisa. Aya hii ya Matendo 1:9 Inasema kwamba, akisha kufufuka, Nabii Isa alichukuliwa Winguni.
Je, Nabii Isa baada ya kuinuliwa hadi mbinguni, alikaa wapi?
Tunaigeukia Qur’an tena kuona ni wapi Nabii Isa anakaa baada ya kuinuliwa hadi mbinguni,
Katika Tafsiri ya Abdallah Farsy Sura ya 3:55 Anamnukuru Az Zamakhshary mwanachuoni mkubwa wa Kiislam katika Tafsri yake anasema
“Kwenye tamko hili ameandika AzZamakhshary kwenye hii Al Kashshaaf yake: Warafaaka ilayya Illaa Samaiy wamaqarri Malaaikaty (Nitakuleta kwangu kweye mbingu zangu, na Mahala wanapokaa Malaika wangu)
Hii inamaana kwamba Nabii Isa aliinuliwa akapandishwa hadi mbinguni, mahali anapokaa Mungu na Malaika zake. Hii inatupatia ushahidi ndani ya Qur’an kuwa nabii Isa ametukuka Sana kuliko Mitume wote, hakuna mwanadamu anayeweza kupewa daraja hii ya juu sana, ya kukaa pamoja na Mungu na Malaika zake. Kwa maana nyingine ni kwamba nabii Isa amepewa heshima ya kuwa pamoja na Mungu. Biblia inawafikiana kabisa na Qur’an juu ya jambo hili la nabii Isa Kupewa kuketi pamoja na Mungu na Malaika zake.
Katika Biblia aya zifuatazo zinaonyesha kuwafiki wazo hili
“Je! Yuko malaika aliyemwambia wakati wo wote, Uketi mkono wangu wa kuume Hata nitakapoweka adui zako chini ya nyayo zako?” (Waebrania 1:13
“Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, Malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake” 1Ptero 3:22
“Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.” Waebarania 12:3
“Basi, , yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.” Wakolosai 3:1
“…Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko mbinguni” Waebrania 1:4
“Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni” Waebrania 8:1
Hivyo twaona ya kuwa, kwa mujibu wa Biblia Takatifu, baada ya kufa, na akafufuliwa kuwa hai, kwa kweli siyo tu kwamba nabii Isa aliinuliwa hadi mbinguni kwa Mungu akakaa pamoja na Malaika, lakini aliketishwa mkono wa kuume katika kiti cha enzi cha Mungu. Yaani, Amekaa sawasawa na Mungu katika kiti chake cha Enzi. Wamekaa kiti kimoja, nabii Isa akiwa mkono wa kuume.
Biblia inaeleza wazi sababu za nabii Isa kuketi katika kiti cha enzi cha Mungu. Tunasoma katika Kitabu cha Waebrania 1:3
“Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”
Ni kwa sababu, Yeye ni mfano wa Mungu (chapa ya Mungu). Hakuna mwanadamu anayeweza kuketishwa katika kiti cha enzi cha Mungu isipokuwa ni yule aliye kama Mungu mwenyewe, mwenye asili ya Mungu. Ni nabii Isa peke yake ambaye anasifa ya kuwa kama Mungu kama maandiko yasemavyo katika kitabu cha Wafilipi 2:6 “…ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu….”
Yeye mwenyewe alipokuwa hapa duniani aliwahi kusema akimwambia Mungu.
“Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako” Yohana 17:5
Tunaona kwamba, siku zote milele na milele, nabii Isa amekuwa na utukufu wa kuwa pamoja na Mungu katika Kiti chake cha Enzi, anapomaliza kazi yake hapa duniani aliyotumwa kuifanya Mungu anamrudishia ule utukufu kwa kumpandisha mbinguni, moja kwa moja kwenye kiti chake cha enzi.
Ndiyo Maana Qur’an katika Sura ya 3:45 inasema;
“...اسْمُهُ الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ وَجِيهًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ”
“…Jina lake ni Masih, Isa mwana wa Maryam mwenye heshima katika dunia na Akhera, na Miongoni mwa waliopelekwa mbele na Mwenyezi Mungu”
Qur’an yaonyeshwa wazi kuwa nabii Isa bin Maryam ana heshima duniani na Akhera (Mbinguni), tena amepelekwa mbele na mwenyezi Mungu, bi maana, mbele kuliko manabii wote, Yeye ni zaidi ya nabii. Ndiyo maana akasema alipokuwa amekaribia kupaa mbinguni
“Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani” Mathayo 28:18
Na katika kitabu cha Wafilipi 2:9-10 tunaambiwa ukubwa wa mamlaka hayo aliyopewa nabii Isa.
“Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;”
Je ni Kazi gani anayoifanya Nabii Isa baada ya kuinuliwa mbinguni?
Hakika haiwezekani kwamba nabii Isa apandishwe mbinguni na aketi bure bila kazi yoyote kwa muda wa zaidi ya miaka 2000 hadi sasa. La sivyo hastahili awe hai. Vitabu vitakatifu vinatueleza ni kazi gani anayoifanya baada ya kupaa Mbinguni.
“Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji” Waebrania 4:14-16
Nabii Isa sasa anasimama kama kuhani wetu Mkuu. Kazi ya kuhani ni kufanya upatanisho na maombezi kwa watu wa Mungu, Biblia inayo maelezo mazuri ya juu ya ukuhani wa Nabii Isa.
“Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa” Waebrania 5:5
“Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee” Waebrania 7:25
“Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” 1Yohana 1:1-2
Nabii Isa ni mwombezi wetu, hii ndiyo kazi anayoifanya toka siku ile alipoinuliwa akapandishwa juu mawinguni , na kuingia mbinguni, aliko Mungu na Malaika. Hakuna mtu awezaye kusamehewa dhambi alizozifanya isipokuwa ataombewa na Nabii Isa, Vitabu vitakatifu vyote vinatufundisha hivyo. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 4:12 tunaambiwa;
“Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”
Nabii Isa mwenyewe aliwahi kujinadi kuwa ni Mwombezi wetu alipokuwa hapa Duniani akisema
“Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;” Yohana 14:15-1
2. USHUHUDA WA WANAFUNZI WA NABII ISA JUU YA KUFA NA KUFUFUKA KWAKE
Jambo lingine tunaloangalia ni ushuhuda unaotolewa na wale ambao walikuwa wafuasi wake wa karibu sana, yaani wanafunzi wake. Hawa ni wale waliotembea naye kila siku akiwa hapa duniani. Kusudi la kufanya wanafunzi ni kwamba Nabii Isa alitaka watu hawa wawe “mashahidi wa mambo haya” Luka 24:48. Eneo lao la kazi hii ya kushuhudia “mambo haya” lilipaswa liwe duniani kote. Aliwaagiza akisema;
“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu”.” Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” Matendo 1:8, Mathayo 28:20
Hayo mambo ni mambo gani ambayo Nabii Isa aliwataka wanafunzi wake kuyashuhudia kwa Ulimwengu? Wanafunzi wenyewe walifahamu ni mambo gani waliagizwa kuyashuhudia. Baada ya Yuda kujinyonga alipokuwa amekwisha kumsaliti Yesu, ilibidi wanafunzi wa Yesu wachague mwingine wa kuziba pengo hilo, Petro anaeleza sifa za mtu huyo, na kutupatia mwanga wa kazi ambayo wanafunzi walipewa na Nabii Isa.
“Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu, kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.”Matendo 1:21-22
Hii ndiyo kazi iliyokuwa imewashughulisha sana Wanafunzi wa Nabii Isa. Mioyo yao ili jaa mzigo wa jambo hili, kushuhudia jinsi Nabii Isa alivyokufa na kufufuka. Hivi ndivyo walivyohubiri na kutangaza kwa watu.
“Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake” Matendo 2:32
Wakishindana na Wayahudi, Waandishi na Mafarisayo waliwashutumu wakisema;
“Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.” Matendo 3:15.
Wanafunzi wa Nabii Isa wakiwa ni wale watu walioambatana naye tokea ubatizo wa Yohana hadi alipopaa kwenda mbinguni, walikuwa ni watu sahihi kushuhudia ulimwenguni kwamba Mwokozi alikufa kwa ajili ya dhambi za watu na kufufuka kama mshindi dhidi ya kaburi, waliendelea kusema;
“…habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi” Matendo 10:38-43.
Hakukuwa na jambo lolote lile ambalo lingewakatisha tamaa kutotanganza kufa na kufufuka kwa Nabii Isa. Hata wakati walipotishiwa na kukatazwa kuhubiri “mambo hayo”, hawakuwa tayari kutii wanadamu wakisema “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”.
“Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu” Matendo 5:28-29
Walikuwa tayari kukikabili kifo kuliko kuzuiliwa kutangaza kufa na kufufuka kwa Nabii Isa. Hakuna mwanadamu aliyetayari kufa kwa ajili ya kutetea uongo. Wengi majambazi, au hata watu waaminifu kwa nchi yao wanapokamatwa na kuteswa wakihojiwa wako tayari kutoa siri zote kuliko kusema uongo. Haiyumkiniki wanafunzi wa Nabii Isa wapoteze maisha yao kwa kutetea uongo. Wengi wao walikufa kwa kushuhudia “mambo hayo” tena vifo vibaya sana. Walikatwa misumeno, wengine walitundikwa mtini kichwa chini miguu juu. Wengine walichomwa moto na vifo vingine vya mateso.
“wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.” Waebrania 11:36-38.
Ikiwa hatuwezi kuyaamini maneno ya mashahidi waliotumwa kushuhudia kwetu juu ya Kifo na ufufuo wa Nabii Isa, wale wanaotuhubiria wakisema “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. 1Yohana 1:3. Basi tuwe na uhakika kwamba ushuhuda mwingine utakaoletwa na Mtu mwingine asiyokuwa na sifa hizo hautakuwa sahihi. Wengi wanaokata kufa na kufufuka kwa Yesu ni wale waliochagua kuwasikiliza mashahidi wengine ambao, hawakumwona wala kumgusa, wala kula na Yesu. Hawafai kabisa mashahidi hao, ni Mashahidi wa Uongo.
3. USHUHUDA WA HISTORIA JUU YA KUFA NA KUFUFUKA KWA YESU.
Tumekwisha kuona vitabu vitakatifu vyote Biblia na Qur’an vyote vinashuhudia jinsi ambavyo kwakweli Nabii Isa (a.s) alikufa na akafufuliwa kuwa hai na kisha akapaishwa kwenda mbinguni. Kwa sababu tukio la kufa kwake msalabani ni tukio ambalo lilikuwa la wazi bila kificho. Bila shaka kusingeweza kukosekana watu wengine walioshuhudia tukio hilo. Katika hili tuchunguze maandishi ya wanahistoria wa Kiyahudi ambao walikuwepo nyakati hizo. Ikumbukwe pia kwamba Wayahudi walimkataa Yesu kama Masihi, hivyo maandiko yao hayana upendeleo wa Ukristo. Na katika hili tumwangalie mwanahistoria mashuhuri wa Kiyahudi, Flavius Josephus.
“Katika wakati huu alikuwepo Yesu, mtu mwenye hekima, ikiwa itakuwa sahihi kumwita mtu; kwa maana alikuwa akifanya maajabu makubwa, mwalimu wa watu waliokuwa wakipokea ukweli kwa furaha, aliwavuta Wayahudi wengi na pia Wayunani wengi. Mtu huyu alikuwa Kristo na wakati Pilata halipomhukumu msalabani…wale waliompenda kutokea mwanzo hawakumwacha, kwa maana aliwatokea tena akiwa hai siku ya tatu…Manaabii watakatifu wakisha kunena hili na mambo mengi kumhusu yeye. Hata sasa jamii ya Wakristo, walioitwa jina hilo kutokana na yeye, haijafa bado.” Antiquities, 18:3,3.
Wanahistoria wa Kirumi wa Karne ya 1 na ya 2
Sambamba na Wayahudi, wengine walioshuhudia tukio la kufa kwa Yesu ni Warumi wenyewe ambao viongozi wao walimhukumu Yesu afe msalabani.
Tacitus: Mwanahistoria wa Kirumi akiandika mnamo mwaka 115 AD anassema juu ya mateso ya Kaisari Nero kwa Wakristo, kwamba;
“Christus, ambapo jina lao limetokana (hao Wakristo) alihukumiwa na Pilato wakati wa kutalwala kwake Tibelio.”
Katika Talmud ya Wayahudi, pia tunasoma kwamba;
“Wakati wa pambazuko la Pasaka alisulubiwa Yesu wa Nazareti”
Je ni kwa nini leo wengi wanapinga juu ya kufa na kufufuka kwa Nabii Isa, Uongo huo ulianzia wapi na lini?
Jambo hili la kupinga kufa na kufufuka kwa Nabii Isa halikuanza leo. Mara tu baada ya kufufuka kwake siku ile ile, kikao kilifanyika kati ya viongozi wa dini ya Kiyahudi na maaskari waliokuwa wakilinda Kaburi lake. Tunasoma katika kitabu cha Mathayo kwamba;
“Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo” Mathayo 28:11-15.
Inashangaza kuona kuwa, mpango wa kukataa kufa na kufufuka kwa Nabii Isa ulioanzishwaa na Wayahudi kwa kushirikiana na maaskari wa Kirumi, ndiyo unaoonekana kukubarika kwa watu maelfu hivi leo. Hivyo inategemea utachagua kumsikiliza nani, Je, ni wanafunzi wa Yesu walioshuhudia tukio la kufa na kufufuka, au viongozi wa dini ya Kiyahudi. Je utachagua kusikiliza kauli ya Nabii Isa mwenyewe ndani ya vitabu vitakatifu, au utachagua kuwasikiliza hao maaskari wa Kirumi.
Vipi Kuhusu Kauli inayopatikana katika Qur’an Sura ya 4:157-158?
وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ. وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ. مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ. وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا. بَل رَّفَعَهُ اللَّهُ إِلَيْهِ. وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا
“Na kwa ajili ya kusema kwao: “sisi tumemwuua Masih Isa mwana wa Maryam, Mtume wa Mungu” hali hawa kumwua wala hawakumsalibu, bali walibabaishiwa (mtu mwengine wakamdhani Nabii Isa). Na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika hakika ya (kumwua) Nabii Isa wamo katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa), wao (kabisa) hawana yakini juu ya (jambo) hili (la kuwa kweli wamemwua Nabii Isa) isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumwua.”
Kutokana na yale tuliyokwisha kuangalia kama ushahidi wa kufa kwa Yesu aya hii kwa haraka haraka yaonekana kupinga kifo cha Yesu. Ikiwa itachukuliwa Kumaanisha hivyo, basi aya hii itaonekana kupinga aya zingine za Qur’an na pia kupinga vitabu vya manabii waliotangulia, na hivyo kupinga hata imani yenyewe ya Kiislamu. Uislamu utasimama na kuanguka kwa aya hii moja. Kwani ikiwa kweli Yesu alikufa na kufufuka kama tulivyoona, halafu aya ndani ya Qur’an ije kupinga miaka 600 baadaye, swali litakuwa ni kweli aya hii inatoka kwa Mungu au ilichomekwa katikati ya Qur’an?
Ukichunguza aya hii kwa kina utagundua kwamba. kuna watu wanaodai kwamba wamemuua Masihi, Je hivi kweli masihi ali uawa na watu tu, tumsikie Yesu mwenyewe anasemaje? Katika Yohana 10:17-18 tunasoma;
“Ndiposa baba anipenda, kwa sababu nautua uhai wangu, ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uwezo wa kuutoa, ninao na uwezo wa kuutwaa tena…”
Hivyo ni kweli kabisa kwamba wale wanaosema kuwa walimuua, kwa kweli hawakumuua, bali aliutoa uhai wake yeye mwenyewe.
Aya pia inasema walibabaishiwa mtu mwingine, wakadhani ya kuwa ndiye Nabii Isa (a.s). Jambo hili la kubabaishiwa mtu mwingine, halikutokea wakati wa utu uzima wake pale alipohukumiwa kufa msalabani, bali jambo hili lilitokea wakati wa utotoni mwake. Yesu alipata jaribio la kuuawa wakati wa utoto. Hii ni wakati ambapo Herode alitoa amri ya kuwaua watoto wote wenye umri chini ya miaka miwili, kama tunavyosoma katika Mathayo sura ya 2:16
“Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mama jusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawauwa watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi”
Wakati huo wa tukio hili ndipo ambapo tunaweza kusema walidhani ya kuwa wamemuua, lakini waliuawa watoto wengine, wakadhani ya kuwa na Nabii Isa (a.s) amekwisha kuuawa. Hivyo walifuata dhana tu “na kwa yakini hawakumuua.” Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amwambia Yusufu kumchukua Mariamu, ili wakimbie kujificha Misri.
“…tazama Malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize” (Mathayo 2:13)
Juu ya tukio hili Qur’an inasema kwamba;
“Na Tukamfanya Mwana wa Mariam na mama yake kuwa ni Ishara, na tukawapa makimbilio kwenda mahali palipoinuka penye utulivu na chemichemi za maji” (Sura 23:50).
Hivyo tukio la kubabaishiwa mtu mwingine wakamuua badala ya Nabii Isa (a.s) lilitokea wakati wa utoto wake Wakati wa amri ya mfalme Herode, na siyo wakati wa msalaba.
Kwa mujibu wa Qurán Sura ya 4:157-158 ni kina nani hao waliohitilafiana juu ya tukio la kufa na kufufuka kwa Nabii Isa?
وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ. وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ. مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ. وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا. بَل رَّفَعَهُ اللَّهُ إِلَيْهِ. وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا
“Na kwa ajili ya kusema kwao: “sisi tumemwuua Masih Isa mwana wa Maryam, Mtume wa Mungu” hali hawa kumwua wala hawakumsalibu, bali walibabaishiwa (mtu mwengine wakamdhani Nabii Isa). Na kwa hakika wale waliokhitilafiana katika hakika ya (kumwua) Nabii Isa wamo katika shaka nalo (jambo hilo la kusema kauawa), wao (kabisa) hawana yakini juu ya (jambo) hili (la kuwa kweli wamemwua Nabii Isa) isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumwua.
Tuangalie tafsir ya Sura ya 3.55 katika Tafsir ya Ibn Kathir
“(Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema “Ewe Isa! Mimi nitakufisha, na nikuinue kwangu. Na nikuepushe na wale waliokufuru, na niwafanye wale waliokufata wawe juu ya wale walio kufuru mpaka siku ya Kiyama…” Sulat Maidah 3:55
إختلف المفسرون في قوله تعالى « إني متوفيك ورافعك إلي » فقال قتادة وغيره هذا من المقدم والمؤخر وتقديره إني رافعك إلي ومتوفيك يعني بعد ذلك وقال علي بن أبي طلحة عن ابن عباس إني متوفيك أي مميتك وقال محمد بن إسحاق عمن لا يتهم عن وهب بن منبه قال توفاه الله ثلاث ساعات من أول النهار حين رفعه إليه قال ابن إسحاق والنصارى يزعمون أن الله توفاه سبع ساعات ثم أحياه قال إسحاق بن بشر عن إدريس عن وهب أماته الله ثلاثة أيام ثم بعثه ثم رفعه
Ibn Kathir anasema kwamba;
“Wamehitilafiana wafasiri wa Qurán juu ya kauli ya Mwenyezi Mungu “mimi nitakufisha na nikuinue kwangu”. Amesema Katada na wengine, ‘Kauli hii ni kutokea mwanzo na kisha mwisho wake na inakadiriwa kwamba ‘mimi nitakuinua kwangu na kisha ndipo nikufishe. yaani, baada ya hayo [yaani ni kwamba wanaifanyia uhariri (editing) kauli ya Mwenyezi Mungu]. Amesema Aliy bin Abiy Twalaha kutoka kwa ibn Abaasi, ‘mimi nitakufisha, yaani nitakufanya kuwa maiti. Amesema Muhammad bin Is-haaka...kutoka kwa Wahab, amesema, Mwenyezi Mungu alimfisha masaa matatu kutoka mwanzo wa mchana kisha akamwinua kwake. Amesema ibn Is-haaka na Manasara wanazani kwamba, Mwenyezi Mungu alimfisha masaa saba kisha akamfufua. Amesema Is-haaka bin Bashir, kutoka kwa Idrisa kutoka kwa Wahab, Mwenyezi Mungu alimfisha siku tatu kisha akamfufua, kisha akamwinua hadi kwake.
Niwazi kwamba kuhusu kufa na kufufuka kwa Nabii Isa, Wanazuoni wa kiislamu wamehitirafiana sana kama anavyoonyesha ibn Kathir, hii inapelekea waislamu kutokuwa na mwafaka juu ya jambo hili la kila kundi kufuata mafundisho yaliyo tofauti na kundi jingine. Hawa ndio Qurán inawataja kwamba, Wanafuata dhana tu! hawana yakini juu ya jambo hili.
Ndiyo maana leo hakuna mwislamu yeyote anauhakika ni nani ambaye waliotaka kumuua Nabi Isa walibabaishiwa.
Ushahidi wa kuhitilafiana kwa wanachuoni wa Kiislam juu ya tukio la kutosulubiwa na kuinuliwa kwa nabii Isa hadi mbinguni.
Kabla hatujahitimisha somo hili, hebu tuziangalie kauli mbali mbali za wanachuoni wa Kiislam juu ya kumpandishwa mbinguni nabii Isa. Ni muhimu kuziangalia kauli hizi ili tuweze kubaini kwamba, iwapo wanachuoni wenyewe wanaeleza matukio yenye kuhitilafiana basi ni wazi kwamba hawana uhakika juu ya jambo hili, wanafuata dhana tu, ya kudhani kuwa hakusulubiwa.
Wafasiri wakubwa wa Qurán kama vile, AtTwabariy, Ibn Kathir na AzZamakshari wote wamenukulu tukio la kuinuliwa juu katika mazingira yafuatayo.
Kisa cha kwanza.
وذهب هو وطائفة من اليهود إلى المنزل الذي فيه عيسى
عليه السلام وهو في جماعة من أصحابه اثني عشر أو ثلاثة عشر وقيل سبعة عشر نفرا وكان ذلك يوم الجمعة بعد العصر ليلة السبت فحصروه هنالك فلما أحس بهم وأنه لا محالة من دخولهم عليه أو خروجه إليهم قال لأصحابه أيكم يلقى عليه شبهي وهو رفيقي في الجنة فانتدب لذلك شاب منهم فكأنه أستصغره عن ذلك فأعادها ثانية وثالثة وكل ذلك لا ينتدب إلا ذلك الشاب فقال أنت هو وألقى الله عليه شبه عيسى حتى كأنه هو وفتحت روزنة من سقف البيت وأخذت عيسى عليه السلام سنة من النوم فرفع إلى السماء وهو كذلك كما قال الله تعالى « إذ قال الله ياعيسى إني متوفيك ورافعك إلي » الآية فلما رفع خرج أولئك النفر فلما رأى أولئك ذلك الشاب ظنوا أنه عيسى فأخذوه في الليل وصلبوه ووضعوا الشوك على رأسه وأظهر اليهود أنهم سعوا في صلبه وتبجحوا بذلك وسلم لهم طوائف من النصارى ذلك لجهلهم وقلة عقلهم ما عدا من كان في البيت مع المسيح فإنهم شاهدوا رفعه وأما الباقون فإنهم ظنوا كما ظن اليهود أن المصلوب هو المسيح ابن مريم
Akaja [msaidizi wa mfalme wa Damaska] na kundi la Mayahudi katika nyumba ambayo ndani yake walikuwemo nabii Isa na wanafunzi wake wapata kumi na wawili au kumi na watatu au kumi na saba. siku hiyo ilikuwa siku ya Ijumaa jioni, wakaizunguka nyumba hiyo. Naye (nabii Isa) alipohisi kwamba wanakaribia kuingia ndani, au kwamba karibuni ataondoka, aliwaambia wanafunzi wake, ni nani anajitolea iliafanywe kufanana nami, naye atakuwa mshirika wangu peponi? Kijana mmoja akajitolea, lakini nabii Isa akaona kwamba kijana huyo ni mdogo sana. Akarudia kuuliza swali hilo mara ya pili na ya tatu na kila mara kijana huyo huyo alikuwa akijitolea. Kisha nabii Isa akasema, basi sawa utakuwa ndiye. Kisha Mwenyezi Mungu akamfanya kijana huyo aonekane na sura kama ya nabii Isa . Wakati huo tundu kubwa likatokeza juu ya dari ya nyumba, na nabii Isa akaletewa usingizi, na kisha akapandishwa mbinguni akiwa amelala...zama alipopandishwa mbinguni nabii Isa, wale waliokuwa ndani ya nyumba wakatoka nje. Na wale waliokuwa wakiizunguka nyumba walipomuona yule anayefanana na nabi Isa, wakamdhania kuwa ndiye nabii Isa. Basi wakamkamata usiku ule, wakamsurubisha na wakamvika taji ya miba kichwani mwake.”
Kisa cha pili.
عن وهب بن منبه قال أتى عيسى ومعه سبعة عشر من الحواريين في بيت فأحاطوا بهم فلما دخلوا عليه صورهم الله عز وجل كلهم على صورة عيسى فقالوا لهم سحرتمونا ليبرزن لنا عيسى أو لنقتلنكم جميعا فقال عيسى لأصحابه من يشري نفسه منكم اليوم بالجنة فقال رجل منهم أنا فخرج إليهم وقال أنا عيسى وقد صوره الله على صورة عيسى فأخذوه فقتلوه وصلبوه فمن ثم شبه لهم فظنوا أنهم قد قتلوا عيسى وظنت النصارى مثل ذلك أنه عيسى ورفع الله عيسى من يومه ذلك
Hadithi ya Wahab bin Munib: amasema, aliingia nabii Isa ndani ya nyumba, pamoja naye watu kumi na saba miongoni mwa wanafunzi wake wakamzunguka. Mwenyezi Mungu aliwawekea sura ya nabii Isa wote. Wakasema (wale wenye kumtafuta nabii Isa), ‘mmetufanyia uchawi, tubainishieni nabii Isa, la sivyo tutawauweni wote. Akasema nabii Isa kuwaambia wanafunzi wake, ni nani miongoni mwenu atanunua pepo kwa nafisi yake leo. Akasema mmoja wao, mimi hapa ndiye nabii Isa. Kisha akatoka kuwaendea, Mwenyezi Mungu alikuwa amemwekea sura ya nabii Isa. Wakamchukua, wakamsulubisha, wakamuua. Walikuwa wamefananishiwa nabii Isa, wakadhani ya kuwa wamemuua nabii Isa. Na Manaswara wakadhani hihi hivyo pia, kuwa alikuwa ni nabii Isa. Na Mwenyezi Mungu akamwinua nabii Isa...” (Rejea Tafsir ya AtTwabariy, Ibn Kathir na AzZamakshari juu ya Sura ya 4:157)
Visa hivi vinaaminika ndani ya wanachuoni wa Kiislam na umati wa Waislam pia kuwa ni visa vya kweli, kiasi ya wanachuoni hawa kuvitumia kujenga hoja ili kuthibitisha kwamba nabii Isa hakusulubiwa wala hakuuawa msalabani. Hebu tutafakari visa hivi.
Tunagundua katika visa hivi matatizo yafuatayo.
1. Tofauti ya Idadi ya wanafunzi wa Yesu aliokuwa nao wakati wa tukio. Mara walikuwa kumi na wawili, mara walikuwa kumi na watutu mara walikuwa kumi na saba. Tushike lipe sasa? Hii ni wazi kwamba hakuna uhakika juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.
2. Kisa cha kwanza tumeona kwamba, ni mmoja tu ndiye aliyefananishwa na baii Isa, lakini kisa cha pili tunaona kwamba ni wote walifaninishiwa sura ya nabii Isa kiasi cha waliokuwa wanamtafuta walichanganykiwa, na ndipo mmoja akajitokeza. Tushike lipi kati ya haya mawili?
3. Katika visa hivi, nabii Isa anawauliza wanafunzi wake, ni nani ajitolee kuuawa badala yake. Jambo hili ni la kushangaza sana! Kwanini Allah afanye ukatiri mkubwa namna hii, wa kumfanya mtu afe bila hatia kwa ajili ya mwingine. Kwanini nabii Isa asichukue mzigo wake mwenyewe? Je Allah ambaye anauwezo wote alishindwa kumwokoa nabii Isa kwa njia yoyote mpaka ujanja wa namna hii ufanyike?
4. Visa hivi viwili vinasema, tukio la mtu fulani kusulubishwa na kuvikwa taji ya miiba (kama lilivyorekodiwa katka Injili) ni hakika lilitokea. Lakini mtu aliye sulubiwa, na kuuawa siye nabi Isa. Kisa kinasema kwamba kupitia vitimbi hivi walivyofanya nabii Isa na Allah, Wakristo walidhani ya kuwa nabii Isa amekufa. Hivyo visa hivi vinamfanya Allah kuwa mwongo. Kwamba iwapo Wakristo wanaamini kwamba Yesu alikufa, ni kwasababu Isa na Allah waliwadanganya. Hii ni kufuru kubwa ya kumfanya Allah aonekane mwongo.
Hivyo ni rahisi sana na inaleta maana na mantinki kubwa kuamini kama isimavyo Biblia kwamba Yesu alikufa na kufufuka kwa ajili yangu na yako, ili kupitia kifo chake tupate kuingia peponi.
Katika somo hili tumeona kwamba Yesu (Nabii Isa) alikufa kwa ajili yako na yangu ili kupitia Kifo chake mimi na wewe tuweze kuokolewa. Kuukubari ukweli huu wa maandiko kutaleta wokovu na mwisho uzima wa milele. Yesu Kristo yu hai sasa mbinguni ili atuombee, “maana yu hai siku zote ili awaombee” Waebrania 7:25. Bwana akubariki kwa kuwa leo hii utamchagua Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa Maisha yako.