Hiki ni Kitabu kisicho kuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachaMungu,”
Hii ni kwa mujibu wa tafsiri ya Quran Tukufu kama ilivyotafsiriwa na Shekhe Abdallah Farsy. Lakini tunaposoma tafsiri ya aya hii katika tafsiri ya Quran kama ilivyotafsiriwa na Waislamu wa Madhehebu ya Ahmadiyya inasema kwamba.
“Hicho ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachaMungu”
Ukichunguza vizuri maneno haya ya Kiswahili, utagundua kwamba kuna tofauti ya maana. Neno lililotumiwa na Abdallah Farsy katika tafsri yake ni “Hiki ni Kitabu”, wakati maneno ya tafsri ya Ahmadiyya ni “Hicho ni Kitabu”. Tofauti hapa ni kwamba, neno hiki linaashiria kitu kilicho karibu (mkononi) wakati ambapo, neno hicho, linaashiria kitu kilicho mbali siyo kilichopo mkononi. Ili kuondoa utata wa utofauti huu wa maneno haya mawili ni vizuri kuangalia neno halisi lililotumika katika lugha ya asili, lugha ya Kiarabu ambayo ndiyo lugha ya Quran.
Neno lililotumika hapa ni ذَٰلِكَ(Dhaalika). Neno hili dhaalika, kwa kiarabu linaitwa “ismu ishaaratu lil bai’di” yaani jina la kuashiria kitu kilicho mbali, maana yake kwa Kiswahili ni “Hicho”.
Neno lingine linalofanana na hili ni هَذَا(Hadha), maana yake ni “hiki”. Kwa hiyobasi tafsiri sahihi ya aya hiyo ni ile inayosomeka ““Hicho ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wacha Mungu”. Hii inamaana kwamba, aya hii haikusudii Quran ni kutokana na historia yenyewe ya uteremsho wa Quran. Inasadikika kwamba, Muhammad alipata utume wake katika mwaka wa 610 AD. Waislamu wanaamini kwamba Wahyi, ama ufunuo kwa Muhammad ulikuja kidogo kidogo. Hii ni ktokana na Qurán yenyewe inavyoejieleza katika sura ya 17:106
وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا
Na Qurán tumeigawa seheme mbali mabli (kwa kuiteremsha kidogo kidogo) ili uwasomee watu kwa kituo; na tumeiteremsha kidogo kidogo (iwe wepese kuhifadhika)
Kwakuwa hakujua kusoma wala kuandika ilibidi akariri maneno aliyofunuliwa, na pia aliwakaririsha masahaba zake.
Muhammad alifariki katika mwaka wa 634 AD. Hadi anafariki hakukuwa na kitabu hiki kiitwacho Quran, bali ujumbe huo ulikuwa umehifadhiwa vifuani mwa masahaba, ambao waliitwa muhafidhuuna (Wenye kuhifadhi), au Qura. Ingawa baadhi ya masahaba wa Mtume Muhammada (s.a.w) waliandika Qurán katika «majalada ya ngozi, mawe, mifupa na vitu vingine», (Shekhe Said Moosa Mohamed Al-Kindy; Mkweli Mwaminifu, Chapa ya 15, Juzuu ya 1-2 uk 18) hakukuwa na sahaba yeyote aliyeweza kuandika Qurán nzima. Muhammad mwenyewe hakuwa anajua kusoma na kuandika kama ilivyorekodiwa katika Qurán 7:158
...فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَا
Basi muaminini Mwenyezi Mungu na mtume wake asiyejua kusoma na kuandika
(Baada ya Muhammad kufariki, alitawala Khalifa (kiongozi) wa Kwanza wa Umma wa Kiislamu aliyekuwa akiitwa, Abbakar Sadik. Yeye aliwaongoza Waislamu katika vita vya Yamama mwaka huo 634. Katika vita hivi, walikufa masahaba wengi waliohifadhi Quran wapatao 70, hivyo kukawa na hofu kubwa ya kupotea kwa Quran iwapo muhafidhuuna wote wange kufa. Hivyo Uthuman bin Afan, swahaba mwingine wa Muhammad, akapendekeza kwa Abbakar kwamba waikusanye Quran na kuiandika.
«Akaambiwa Sayyidina Abu Bakar (Radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake) akakataa, akasema mbona mnanitwika mzigo huu mimi?» (Mkwweli Mwaminifu uzuu 1-2 uk 15)
Imamu Bukhariy anaelezea kukataa kwa Abu Bakari kuifanya kazi hii ya kuikusanya Qurán katika msahafu mmoja akinukuru hadithi ya Zaid bin Thabit Al-Ansari kwamba;
“...قَالَ أَبُو بَكْرٍ قُلْتُ لِعُمَرَ كَيْفَ أَفْعَلُ شَيْئًا لَمْ يَفْعَلْهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم”
Abu Bakar akasema, nitafanyaje kazi ambayo mtume mwenyewe hakuifanya? (Sahihi Bukhari Juzuu ya 6 hadith na. 201)
Maneno haya ya Abu Bakar yanaonyesha wazi kwamba, kamwe Muhammad hakuamurisha masahaba kukusanya Qurán na mpaka kifo chake haikuwa imekusanywa katika msahafu mmoja.
Ndipo Abbakar akachagua kamati ya watu 12 ikiongozwa na Zaid ibn Thabit. Pamoja naye walikuwepo katika kamati hiyo, Uthman ibn Affan, Ali ibn Abi Talib, Talha ibn Ubaydullah, Abdullah ibn Masood, Ubayy ibn Kab, Khalid ibn al-Walid, Hudhaifah na Saliim.
Kamati hii ndiyo kwa mara ya kwanza ikawaitisha masahaba wote waliokuwa wamehifadhi Quran na kila mmoja alisema aya aliyohifadhi. Ndipo watu hawa wakaandika aya hizo na ikapatikana hii Quran yenye Sura 114 na aya 6,236 na maneno yapatayo 323,000.
Kufuatia historia hii, ni uwazi kwamba, hakukuwa na kitabu cha Quran wakati wa Muhammad, kwa hiyo aya hii ya Sura ya 2:2 haiwezekani kabisa kuwa ilikusudia Quran (ambayo haikuwepo wakati huo).
Je, Quran sura ya 2:2 inakusudia kitabu gani hasa?
Ni wazi kwamba wakati wa Muhammad kilikuwepo kitabu tayari kilichoandikwa chenye kukusanya maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo yalifunuliwa kwa manabii wa kale.
Muhammad mwenyewe aliambiwa katika Quran.
قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّهِ ۚ فَإِن تَوَلَّوْا فَقُولُوا اشْهَدُوا بِأَنَّا مُسْلِمُونَ
“Sema: Enyi Watu wa Kitabu! (cha Mwenyezi Mungu. Mayahudi na Manasara) Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; …..” (Quran Sura 3:64)
Hii inaonyesha kwamba, tayari kulikuwa na kundi la watu ambao waliitwa WATU WA KITABU, na kamba kitabu hicho ni “cha Mwenyezi Mungu”, hii ikiwa na maana kwamba walikuwa na kitabu chenye maneno ya Mwenyezi Mungu. Na watu hao ni Mayahudi na Manasara (yaani Wakristo)
Je Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu walichokuwa nacho Mayahudi na Masanara ni kipi?
Katika Quran sura ya 2:113 Tafsiri ya Shekhe Ali Muhsin Al-Barwan wa Madhehebu ya Suni tunasoma kwamba;
وَقَالَتِ الْيَهُودُ لَيْسَتِ النَّصَارَىٰ عَلَىٰ شَيْءٍ وَقَالَتِ النَّصَارَىٰ لَيْسَتِ الْيَهُودُ عَلَىٰ شَيْءٍ وَهُمْ يَتْلُونَ الْكِتَابَ ۗ كَذَٰلِكَ قَالَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ مِثْلَ قَوْلِهِمْ ۚ فَاللَّهُ يَحْكُمُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ
Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasiojua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana. (Quran Sura 2:113
Hivyo ni wazi kwamba wakati wa Muhammad kilikuwepo kitabu ambacho kitabu hicho ni cha Mwenyezi Mungu, nacho Shekhe Barwan anasema kinaitwa Biblia.
Je Mashekhe na Wanachuoni wakubwa ndani ya Umma wa Kiislamu wanatafsri kuwa Sura ya 2:2 inakusudia kitabu gani kisichokuwa na shaka?
Tuangalie baadhi ya Mashekhe wengine wanasemaje kuhusu aya hii.
Tafsiri ya Ibn Kathiyr juu ya Sura ya 2:2
وقد ذهب بعض المفسرين فيما حكاه القرطبي وغيره أن ذلك إشارة إلى القرآن الذي وعد الرسول صلى الله عليه وسلم بإنزاله عليه أو التوراة أو الإنجيل أو نحو ذلك في أقوال عشرةا
Ibn Kathiyr anasema; Baadhi ya wafasiri kama vile wale waliotajwa na imam Kurtuby na wengine kwamba neno dhaalika, linaashiria Quran iliyoshushwa kwa mtume Muhammad s.a.w ua Taurati au Injili na nyingine kama hizo.
Tafsiri At-Twabariy juu ya Sura ya 2:2
وَقَدْ قَالَ بَعْضهمْ : { ذَلِكَ الْكِتَاب } يَعْنِي بِهِ التَّوْرَاة وَالْإِنْجِيل , وَإِذًا وَجْه تَأْوِيل ذَلِكَ إلَى هَذَا الْوَجْه فَلَا مُؤْنَة فِيهِ عَلَى مُتَأَوِّله كَذَلِكَ لِأَنَّ « ذَلِكَ « يَكُون حِينَئِذٍ إخْبَارًا عَنْ غَائِب عَلَى صِحَّة
Baadhi ya Wafasiri wa Quran wamesema neno “dhaalika l-Kitaab”, yaani ni Taurati na Injili.
Hivyo basi tunaona kwamba wanachuoni wa Kiislamu wamekhitilafiana juu ya ni kitabu gani hasa kisichokuwa na shaka kilichokusudiwa katika Sura ya 2:2 ndani ya Quran. Baadhi wanadai kitabu hicho ni Quran, na baadhi wanasema kuwa kitabu hicho ni Tautati na Injili yaani Biblia.
Kutokana na maelezo hapo juu, yaani tunapochunguza lugha asili ya Kiarabu juu ya neno lililotumika dhaalika, na tunapoangalia historia ya Quran, pamoja na tafsiri za baadhi ya wanachuoni wa Kiislamu, ni dhahiri kwamba; Kitabu kisichokuwa na shaka kilichokusudiwa katika sura ya Quran Sura ya 2:2 ni Biblia Takatifu.
Je twaweza kuiamini Biblia?
Leo hii wengi wanatiliam mashaka usahihi wa Biblia, Wengi hawaamini kama Biblia ni maneno ya Mungu, baadhi ya watu wanadhani kwamba Biblia ni kitabu tu kinachoelezea historia ya wana wa Israeli, na visa vya watu na wafalme mbalimbaali wa kale. Baadhi wanaamini kwamba kumewahi kuwa na Maandiko sahihi ya Mungu hapo zamani kamavile Torati ya Musa, Zaburi ya Daudi, na Injili ya Bwana Yesu, lakini sasa maandiko hayo yameharibiwa na watu na hivyo si ya kuamini tena. Hoja wanayo jaribu kujenga hapa ni kwamba; tunafahamu wazi kwamba Mungu alituma manabii na kuwapatia vitabu ambavyo vilihifadhi neno lake, kwa mfano wanasema, Musa alipewa Torati, Daudi alipewa Zaburi na Yesu alipewa Injili Takatifu na Muhammad akapewa Furkan. Sasa swali la Msingi huwa ni kwamba je, hii Biblia alipewa nabii gani? Hoja nyingine inayoletwa na watu wenye kutilia mashaka Biblia ni kwamba, hata kama Biblia ina maneno ya Mwenyezi Mungu, si kwa usahihi wote kwani yawezekana kabisa kwamba maneno hayo yameharibiwa au kuchafuliwa.
Tutajifunza kuhusu Biblia yenyewe hasa ni nini na ilitoka wapi? Je imetufikiaaje sisi leo? Usahihi wa kitabu hiki kiitwacho Biblia, na pia ikibidi tutaleta mashahidi wa mambo haya kwa kuwa tunaambiwa katika Kumb. 19:15 na Math. 18:16 “Jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu”
Je Biblia ni nini hasa?
Neno hili Biblia, siyo neno la Kiswahili, bali ni neno la Kiyunani (Kigiriki) yaani biblia. Neno hili kwa Kiyunani ni wingi wa neno biblos, ambalo lina maana ya gombo. Hivyo biblia ni mkusanyiko wa magombo ambayo yalitumika zamani kuandikia. Watafsiri wa Biblia walitumia neno hilo hilo kumaanisha kwamba Biblia si kitabu kimoja bali ni mkusanyiko wa vitabu vingi. Biblia ni mkusanyiko wa vitabu vipatavyo 66, vilivyogawanyika katika sehemu mbili yaani Agano la kale vitabu 39 na Agano Jipya vitabu 27.
Kabla ya Yesu, vitabu hivi viligawanyika kutokana na waandishi wake. Kwa mfano, vitabu vilivyoandikwa na nabii Musa jumla vitabu 5 viliitwa Torati ya Musa. Kisha kulikuwa na manabii wengine walioandika vitabu kama jinsi walivyofunuliwa ufunuo na Mwenyezi Mungu. Vitabu vyao vilikusanywa kundi moja na kuitwa Manabii. Kisha sehemu ya mwisho ya mgawanyiko huu iliitwa Zaburi iliyoandikwa na Daudi. Hivyo mtu aliweza kusema Torati, Zaburi na Manabii, kumaanisha Biblia nzima ya wakati huo. (Tazama Luka 23:27, 44).
Yesu alipokuja hapa duniani, mafundisho yake yalikusanywa na kuunda mkusanyiko mwingine wa vitabu ujulikanao kama Injili. Vitabu vinne viliweza kupatikana na kuitwa majina kutokana na wakusanyaji wa mafundisho hayo ya Yesu. Mitume wa Yesu ambao pia walipewa uvuvio kwa njia ya Roho Mtakatifu kama ilivyokuwa ahadi ya Yesu (Tazama Luka 24:49 na Matendo 1:8) waliweza kuandika kundi lingine la mkusanyiko wa vitabu lijulikanalo kama nyaraka. Quran inathibitisha katika Sura ya 5:111 kwamba wanafunzi wa Yesu walipewa ufunuo (Wahyi) na Mwenyezi Mungu.
وَإِذْ أَوْحَيْتُ إِلَى الْحَوَارِيِّينَ أَنْ آمِنُوا بِي وَبِرَسُولِي قَالُوا آمَنَّا وَاشْهَدْ بِأَنَّنَا مُسْلِمُونَ
«Na tulipowafunulia wanafunzi (wako) kwamba: Niaminini na Mtume wangu (huyu Isa)...»
Hivyo tunaweza kuwa na ujasiri wa kusema kuwa maandiko yao waliyoandika ni Wahyi (Ufunuo) wa Mwenyezi Mungu. Maandiko hayo yalikuwa kwa mfumo wa Nyaraka mbali mbali zilizotumwa kwa makanisa ambako wanafunzi hao walihudumu. Hii ilikamilisha sehemu ya Biblia ijulikanayo leo kama Agano Jipya.
Je Vitabu hivi vya Biblia vilipatikanaje?
Ufunuo wa Mungu kwa Wanadamu:-
Hapo mwanzo kabla ya dhambi kuingia duniani, Mungu alizungumza na watu ana kwa ana, mfano tazama Mwanzo 2:15,19. Lakini dhambi ilipoingia duniani, kulitokea utengano kati ya Mungu na Mwanadamu. Tunaona katika Mwanzo 3:9-10 mwanadamu anajificha usoni pa Mungu na Mungu Mwenyewe akaamua kumfukuza atoke usoni pake Mwanzo 3:24. Mungu mwenyewe anasema katika Isaya 59:2 “Lakini maovu yenu yemewatenga ninyi na Mungu wenu, dhambi zenu zimewaficha ninyi uso wake, ili asisikie.”
Hivyo Mungu akatafuta njia nyingine mbadala ya kuwasiliana na wanadamu na hii ni njia ya manabii. Tunasoma katika Waebrania 1:1 “Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali.” Pia tunaambiwa kwamba “BWANA alimtumia nabii kumpandisha Israeli kutoka Misri, kwa njia ya nabii alimtunza.” Hosea 12:13
Je nabii ni nani?
Tunasoma katika 1Samweli 9:9
“Zamani katika Israeli, kama mtu alikwenda kuuliza neno kwa Mungu, angalisema, “Njoo na twende kwa mwonaji, kwa sababu nabii wa wakati huo alikuwa akiitwa mwonaji»
Tunaona hapa kwamba nabii ni mwonaji, kwa maana ya kwamba huweza kuona na kuhabarisha mambo ya usoni ambayo hayajatokea bado. Mungu analo kusudi la kufunua mapenzi yake ya siku za usoni kwa watu wake.
“Mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine, Mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine aliye kama mimi. Nitangazaye mwisho tangu mwanzo, naam, tangu zamani za kale, mambo ambayo hayajatendeka” Isaya 46:9-10.
“Hakika BWANA hatafanya neno lolote bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Amosi 3:7
Hivyo karama ya unabii ndiyo njia sahihi na yenye mamlaka ya juu ambayo Mungu alichagua kuwasiliana nasi. Kupitia njia hii ya manabii Mungu huongea na watu wake. Maneno yanayotoka kwa manabii ni maneno ya Mungu na siyo maneno ya manabii. Yawezekana manabii wakawa na madhaifu ya kibinadamu, hii haimanishi kwamba ujumbe wao una mapungufu. Mara kwa mara manabii walitangaza kwa watu asili ya ujumbe wao wakisema “Neno la Bwana likaniijia”, “Bwana asema”, “lisikieni neno la Bwana”. Wakati mwingine Mungu alitawala midomo ya manabii walipozungumza maneno, mfano Ezekieli 3:26,27; Isaya 50:4-5; 57:19. Hawa manabii wa Mungu waliongozwa na Roho wa Mungu kunena. 1Petro 1:20-21
Mungu alipowapatia manabii ufunuo wake aliwaamurisha kuandika maneno hayo. Tunaona Mungu akitoa amri hii ya kuyaandika maneno katika kitabu tunaposoma kwa mfano katika Kutoka 34:27 Musa aliaambiwa aandike, kadhalika Yoshua (Yoshua 8:32,34;24:26), Daniel (Daniel 7:1), Isaya (Isaya 30:8), Habakuki (Habakuki 2:2), Yeremia (Yeremia 36:2,30:2) Yohana (Ufunuo 1:10-11) na manabii wengine.
Hii yaonyesha kwamba manabii wa Mwenyezi Mungu walijua kusoma na kuandika. Kamwe hakukuwa na nabii wa Mwenyezi Mungu asiyejua kusoma na kuandika. Mungu alikusudia hivyo ili kwamba neno lake lisije likaharibiwa. Kama nabii asingejua kusoma na kuandika uwezekano mkubwa ungekuwapo mwandishi wake kuandika mambo ambayo nabii hakuyatamka kwake na nabii huyo asigundue.
Neno la Mungu lililoandikwa na Musa na manabii wengine likawa ndiyo njia pekee ambayo Mungu alijidhihirisha kwa Israeli na kwa mataifa yote. Ilikuwa ni mpango wa kimbingu kwamba vitabu hivi vitasomwa na kusikiwa na mataifa yote katika vizazi vijavyo ili kwamba watu wamjue Mungu kama Muumbaji na Mwokozi kwa kutii neno lake wapate mibaraka. (Tazama Yoshua 1:8).
Maandiko hayo ya manabii yalikusanywa pamoja na kuitwa BIBLIA, yaani mkusanyiko wa vitabu vya manabii wa Mwenyezi Mungu.
Je Biblia yaweza kuaminika.
“Mwaminini BWANA Mungu wenu hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa” 2Nyakati 20:20.
Ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watu wake siku zote umekuwa “wasadikini Manabii”
Tunasoma pia katika Qurani 2:136 kwamba
قُولُوا آمَنَّا بِاللَّهِ وَمَا أُنزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَمَا أُوتِيَ النَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ
“Semeni: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na tulichoteremshiwana alichoteremshiwa Ibrahimu, na Ismaili na Is’haka na Yakub na Wajukuu na alichopewa Musa na Isa, na walichopewa manabii wote na Mola wao. Hatutofautishi baina ya mmoja wao, na sisi ni wenye kumnyenyekea yeye”.
Mwenyezi Mungu hapendi tuvitilie mashaka vitabu vyake. Ni dhambi kubwa kutilia mashaka vitabu vya Mwenyezi Mungu na kuwaongoza watu kufanya hivyo. Tunaambiwa katika Quran 32:22 kwamba
“Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa aya za Mola wake kisha akazikataa? Hakika sisi ni wenye kuchukua kisasi kwa waovu”.
Mungu anachukua kisasi kwa waovu wanaokataa maneno yake au kuyatilia mashaka. Ikiwa tumeona katika vitabu kwamba vitabu hivi viliandikwa na manabii waliopokea uvuvio kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi kutilia mashaka ni sawa na kujitakia kisasi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa kuzingatia ushauri tuliopewa katika Kumb. 19:15 na Math. 18:16 ya kwamba
“Jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu”
Basi tutaleta mashahidi mbali mbali ili kushuhudia juu ya usahihi wa Biblia.
Shahidi wa Kwanza: Manabii wa Mwenyezi Mungu.
Hebu tuangalie manabii wa Mwenyezi Mungu, je kuna nabii yeyote alipokuja akatia mashaka juu ya Maandiko ya nabii mwenziye aliyemtangulia au ya manabii wengine waliotangulia? Kabla ya yote tunataka kuthibitisha ukweli huu, kwamba “Roho za Manabii huwatii Manabii” 1Wakorintho 14:32. Nabii yeyote wa kweli wa Mwenyezi Mungu hawezi kuwapinga manabii waliomtangulia. Hii ni kwa sababu, Roho aliyewavuvia manabii waliotangulia ni Roho huyo huyo anaye wavuvia manabii wa Mwenyezi Mungu. Kinyume chake iwapo atazuka nabii kuwapinga manabii waliotangulia, tuwe na uhakika kabisa kwamba huyo siyo nabii wa Mwenyezi Mungu.
Imani ya Manabii juu ya Biblia:
Nabii Yoshua na Imani juu ya Maandiko Matakatifu
Huyu ni Nabii aliyefuata baada ya Musa, Je yeye alikuwa na hofu yoyote ya Maandiko ya Torati ya Musa? Hapana, bali aliamini Torati ya Musa kuwa ni Maneno ya Mungu. Tunaambiwa katika Yoshua 8:35 kwamba “Hakuna neno lo lote katika yale yote ambayo Musa alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakulisomea kusanyiko lote la Israeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto na wageni walioishi miongoni mwao”
Mwenyezi Mungu mwenyewe alimwambia Yoshua kulishika neno kama lilivyoandikwa na Musa katika Torati. Yoshua 1:8 “Usiache kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake”.
Baada ya miaka mingi kupita tunaambiwa katika kitabu cha Wafalme 22 kwamba Nabii Hilkia alikiona kitabu cha Torati ndani ya Hekalu na hakuwa na shaka nacho, kisha alikipeleka kwa mfalme, na mfalme akapiga mbiu kuwakusanya watu waje kukisikia kikisomwa masikioni mwao (Soma 2Falme 22 hadi 23)
Daudi na Imani juu ya maandiko matakatifu
Aliamini yote yaliyonenwa katika Torati na sehemu nyingi katika Zaburi yake ananukuu Torati. Kwa mfano Zaburi 77 hadi 78
Yesu na Imani juu ya maandiko matakatifu
Yesu Mwenyewe alipokuja baada ya miaka mingi katika mafundisho yake hatuoni mahali popote akipuuzia Maandiko Matakatifu ya manabii waliomtangulia. Mahali fulani aliwalaumu watu wanaopuuzia Maandiko matakatifu akisema “Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu”. Kumbe kuyapuuzia maandiko ni kujiletea upotevu. Shetani kwa kulijua hili atawaongoza watu kuyapuuzia maandiko ili wapotee.
Katika mafundisho yake mengi Yesu aliwasisitiza watu kusoma maandiko ama yeye mwenyewe kunukuu sehemu nyingi za Maandiko ya maanabii. Mfano ni katika aya zifuatazo.
Marko 12:26 linganisha na Kutoka 33:2-6, Luka 4:17 linganisha na Isaya 61:1-2 Mariko 12:10 linganisha na Zaburi 118:22-23, Yohana 7:48 linganisha na Isaya 44:3 Yohana 13:18 linganisha na Zaburi 41:9
Hizi ni aya chache tu ndani ya Biblia zinazonyesha jinsi Yesu alivyothamini maandiko Matakatifu. Ikiwa hadi wakati wa Yesu Maandiko matakatifu yalikuwa sahihi kiasi cha Yesu Mwenyewe kuyatumia katika maafundisho yake, iweje leo watu wengine wazuke kutupotosha eti Maandiko ya Mungu hayako sahihi. Hakika hii ni mbinu ya mwovu Ibilisi kuwakosesha watu. Yesu aliwahi kufundisha kwamba, usomaji wa maandiko Matakatifu huongoza kwenye uzima wa milele. Yohana 5:39.
“Mwayachunguza maandiko…kwasababu…mna uzima wa milele ndani yake…”.
Ni ujanja wa Shetani kuwaongoza watu kuyapuuza Maandiko Matakatifu ili waukose uzima wa milele.
Shahidi wa Pili: Quran Tukufu.
Mtume Mhammad S.A.W na Imani juu ya Maandiko Matakatifu.
Muhammad S.A.W alizaliwa katika mwaka wa 570 BK na anadaiwa kuwa alipata utume wake katika mwaka wa 610 BK. Hadi kufikia wakati huo tunaweza kupata ushahidi kwamba Biblia ilikuwa sahihi kabisa isiyo na mashaka ndani yake. Hii ni kwa sababu, Muhammad mwenyewe alifunuliwa yakuwa
“Kama watu wa Kitabu (Wayahudi na Wakristo) wangeamini na kumcha (Mwenyezi Mungu) bila shaka tungaliwafutia makosa yao na kuwaingiza katika bustani zenye neema. Na kama wangelisimamisha Taurati na Injili na yale yaliyoteremshwa kwao kutoka kwa Mola wao, hakika wangelikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao, wako watu miongoni mwao washikao njia njema…” Qurani 5:65-66
Kwa mujibu wa aya hii ni wazi kuwa Muhammad S.A.W anabainishiwa kwamba, kama watu wa kitabu watasimamisha Taurati na Injili na yote yaliyoteremshwa kwao wangeweza kuneemeka. Haiwezekani Mwenyezi Mungu amletee Muhammad maneno haya iwapo hadi kufikia wakati wake Biblia ingekuwa imechafuliwa au kutiwa mikono kama watu wanavyodai sasa.
Kisha Muhammad akaendelea kufunuliwa ya kwamba awasisitize watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo) kusimamisha Taurati na Injili.
“Sema: Enyi watu wa Kitabu! Hamna chochote mpaka msimamishe Taurati na Injili (maana yake wafanye kama isemavyo Torati na Injili) na yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu” (kwa maana ya Maandiko ya manabii wengine) Qurani 5:68.
Na ndipo akahitimisha kwa kusema wale Mayahudi na Wakristo wafanyao vitendo vizuri hawatakuwa na hofu wala hawatahuzunika.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالصَّابِئُونَ وَالنَّصَارَىٰ مَنْ آمَنَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ
“Hakika walioamini, na Mayahudi na Masabihi, na Wakristo watakao mwamini Mwenyezi Mungu, na siku ya Mwisho, na wakafanya amali njema, basi wao hawatakuwa na hofu wala hawatahuzunika” Qurani 5:69
Ni dhahiri kwamba Biblia ilikuwa ikingali sahihi hadi wakati wa Mtume Muhammad S.A.W.
Kupitia ufunuo aliopewa Muhammad S.A.W aliwafundisha wafuasi wake akisema
“Wala msibishane na watu wa Kitabu ila kwa yale yaliyobora, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tunaamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyotelemshwa kwenu, na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja nasi ni wenye kunyenyekea kwake” Qurani 29:46.
Hapa ni wazi kwamba Qurani inasisitiza waumini kuamini yale yote ambayo watu wa kitabu walipewa yaani, Taurati, Zaburi, Injili na Manabii wengine. Haiwezekani Mtume Muhammad awaambie watu wake kusema “tunayaamini yaliyoteremshwa kwenu” ikiwa Torati na Injili vingekuwa vimechafuliwa.
Katika Quran, hakuna hata aya moja inayosema kwamba, Taurati, Injili na Zaburi virikuwa vimeharibiwa hadi kuja kwa Muhammad. Badala yake ndani ya Quran kumejaa maneno yanayoonyesha kuwa Vitabu hivi ni ufunuo sahihi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
“Hakika tulitelemsha Taurati yenye muongozo na nuru, ambayo kwayo Manabii waliojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu waliwahukumu Mayahudi na watawa na maulamaa, kwa sababu waliktakiwa kuhifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na walikuwa mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali mniogope (Mimi), wala msiuze aya zangu kwa bei ndogo na wasio hukumu kwa yale aliyoteremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio Makafiri” (Sura 5:44)
“Na tukamfuaatisha Isa bin Maryam katika nyao zao, kuyahakikisha yaliyokuwa kabla yake katia Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake muongozo na nuru inyaosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Tautati na muongozo na mawaidhsa kwa wenye kumcha” (Sura 5:46)
Ni wazi kutokana na aya hizi kwamba Taurati na Injili ni nuru kwa ajili ya wale wamchao Mwenyezi Mungu. Ikiwa watu wanatokea na kukuambia usiziamini tena Taurati na Injili, ni hakika watu hawa wanakunyang’anya nuru aliyotupatia Mwenyezi Mungu na wanataka utembea gizani na Mwisho utaangamia katika moto.
Katika Sura ya 5:46 tumeona kwamba, nabii Isa alikuja kusadikisha yaliyokuwa kabla yake, yaani Taurat na Injili. Mafundisho ya Nabii Isa (Yesu) yanaonyesha kuwa hadi kufikia wakati wake, Taurat na Zaburi vilikuwa sahihi kiasi cha yeye mwenyewe kusema.
“Mwayachunguza maandiko…kwasababu…mna uzima wa milele ndani yake…”. Yohana 5:39
Yesu alifundisha kwamba, Taurat, Zaburi na Manabii haviwezi kutanguliwa (kubadilsishwa), mpaka mbingu na nchi zitakapopita;
“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana amin, nawaambia, mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Mathayo 5:17-18
Itakuwa vyema kusikiliza maneno ya Mwenyezi Mungu kuliko kufuata matamanio ya watu wanaojaribu katika nyakati hizi kutuchanganya na kutugombanisha. Ni hakika kwamba yeyote anayefundisha kuwa Biblia si kitabu cha Mwenyezi Mungu huyo anajikinai mwenyewe nafsi yake na kusudi lake ni kuwapotosha watu. Huyo ameikana imani wala haamini kitabu chochote, kwani kusema hivyo ni kupingana hata na Qurani yenyewe.
Shahidi wa Tatu: Sunna za Mtume Muhammad S.A.W
Mtume alitumia Torati, Zaburi na Injili katika mafundisho yake na pia alihukumu kwa vitabu hivyo. Hapa ni baadhi ya mifano michache tu kuonyesha Muhammad hakuwa na mashaka juu ya vitabu vilivyotangulia.
حَدَّثَنِي مُحَمَّدُ بْنُ بَشَّارٍ، حَدَّثَنَا عُثْمَانُ بْنُ عُمَرَ، أَخْبَرَنَا عَلِيُّ بْنُ الْمُبَارَكِ، عَنْ يَحْيَى بْنِ أَبِي كَثِيرٍ، عَنْ أَبِي سَلَمَةَ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، قَالَ كَانَ أَهْلُ الْكِتَابِ يَقْرَءُونَ التَّوْرَاةَ بِالْعِبْرَانِيَّةِ وَيُفَسِّرُونَهَا بِالْعَرَبِيَّةِ لأَهْلِ الإِسْلاَمِ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم » لاَ تُصَدِّقُوا أَهْلَ الْكِتَابِ، وَلاَ تُكَذِّبُوهُمْ وَقُولُوا {آمَنَّا بِاللَّهِ وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْنَا وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْكُمْ} ». الآيَةَ.
“Imepokelewa kutoka kwa Ubu Huraira: amesema, watu wa Kitabu walikuwa wakisoma Taurati kwa Kiebrania na wakawatafasiria Waislamu kwa Kiarabu. Mjumbe wa Allah akasema (kuwaambia Waislamu), msiwaakubalie watu wa Kitabu, wala msiwakatalie, lakini semeni ‘Tumemwanini Mwenyezi Mungu na yale yaliyofunuliwa kwetu na yale yaliyofunuliwa kwenu” Sahihi Bukhari Hadithi na. 7362
Hadithi hii yaonyesha kwamba, hadi wakati wa Muhammad, Taurati ilikuwa sahihi kiasi cha Muhammad kuwaambia waafuasi wake waiamini
Katika Sahihi Bukhari Juzuu ya 4 hadithi namba 3635 tunasomba;
حَدَّثَنَا عَبْدُ اللَّهِ بْنُ يُوسُفَ، أَخْبَرَنَا مَالِكُ بْنُ أَنَسٍ، عَنْ نَافِعٍ، عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عُمَرَ ـ رضى الله عنهما ـ أَنَّ الْيَهُودَ، جَاءُوا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَذَكَرُوا لَهُ أَنَّ رَجُلاً مِنْهُمْ وَامْرَأَةً زَنَيَا فَقَالَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ” مَا تَجِدُونَ فِي التَّوْرَاةِ فِي شَأْنِ الرَّجْمِ ”
. فَقَالُوا نَفْضَحُهُمْ وَيُجْلَدُونَ. فَقَالَ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَلاَمٍ كَذَبْتُمْ، إِنَّ فِيهَا الرَّجْمَ. فَأَتَوْا بِالتَّوْرَاةِ فَنَشَرُوهَا، فَوَضَعَ أَحَدُهُمْ يَدَهُ عَلَى آيَةِ الرَّجْمِ، فَقَرَأَ مَا قَبْلَهَا وَمَا بَعْدَهَا. فَقَالَ لَهُ عَبْدُ اللَّهِ بْنُ سَلاَمٍ ارْفَعْ يَدَكَ. فَرَفَعَ يَدَهُ فَإِذَا فِيهَا آيَةُ الرَّجْمِ. فَقَالُوا صَدَقَ يَا مُحَمَّدُ، فِيهَا آيَةُ الرَّجْمِ. فَأَمَرَ بِهِمَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَرُجِمَا. قَالَ عَبْدُ اللَّهِ فَرَأَيْتُ الرَّجُلَ يَجْنَأُ عَلَى الْمَرْأَةِ يَقِيهَا الْحِجَارَةَ.
Amesimulia Abdullah bin Umar: Wayahudi walikuja kwa mjumbe wa Allah na kumwambia kwamba, mwanamme mmoja na mwanamke kutoka miongoni mwao alifanya uzinzi. Mjumbe wa Allah akawauliza, “Je mmekuta imeandikwaje katika Torati juu ya adhabu ya Ar-Rajm (kuponda mawe)?” Wakajibu, “tunatangaza kosa lao kisha tunawachapa viboko. Abdullah bin Sam akasema “nyie ni waongo; Torati ina amri ya Rajm”. Wakaleta na kufungua Torati, na mmoja wao akaweka mkono juu ya aya ya Rajm na akasoma aya iliyokuwa kabla yake na ile iliyofuata. Abdullah bin Sam akasema, “ondoa mkono wako”, alipoondoa mkono wake, Aya ya Rajm ilikuwa imeandikwa hapo. Kisha wakasema, “Muhammad amesema kweli; Torati inayo aya ya Rajm. Kisha Mtume akatoa amri kwamba wote wapigwe mawe hadi kufa. (Abdullha bin Umar akasema, “Nilimwona mwanamme akilala juu ya mwanamke ili kumkinga asipigwe mawe”).
Kisha Mwenyezi Mungu akateremushia aya hizi;
Na watakuwekaje kuwa hakimu na wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu? Kisha baada ya hayo wanakataa, na hao si wenye kuamini (Sura 5:43). Hapa tunaona kuwa hadi wakati wa Muhammad, torati ilikuwa sahihi kiasi cha kutegemewa katika hukumu, na Mwenyezi Mungu anamwonyesha mtume kuwa Torati ni sahihi.
Hadithi zifuatazo zinaonyesha Muhammad alikuwa akitumia Biblia katika Mafundisho yake.
حَدَّثَنَا مُعَاذُ بْنُ أَسَدٍ، أَخْبَرَنَا عَبْدُ اللَّهِ، أَخْبَرَنَا مَعْمَرٌ، عَنْ هَمَّامِ بْنِ مُنَبِّهٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ » قَالَ اللَّهُ أَعْدَدْتُ لِعِبَادِي الصَّالِحِينَ مَا لاَ عَيْنٌ رَأَتْ، وَلاَ أُذُنٌ سَمِعَتْ، وَلاَ خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بَشَرٍ »
“Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (r.a): Amesema Mtume (s.a.w), Allah amesema, ‘nimewaandalia waja wangu, mambo (mazuri) ambayo, jicho halijawahi kuona, wala sikio halijapata kusikia, wala moyo wa mwanadamu hauwezi kufikiria”
Linganisha maelezo haya na Biblia:
“Lakini kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halijawahi kuona, wala sikio halikuyasikia, (wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao” 1Wakorintho 2:9
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ يَقُولُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: يَا ابْنَ آدَمَ مَرِضْتُ فَلَمْ تَعُدْنِي. قَالَ يَا رَبِّ كَيْفَ أَعُودُكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ . قَالَ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّ عَبْدِي فُلَانًا مَرِضَ فَلَمْ تَعُدْهُ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّكَ لَوْ عُدْتَهُ لَوَجَدْتَنِي عِنْدَهُ .يَا ابْنَ آدَمَ اسْتَطْعَمْتُكَ فَلَمْ تُطْعِمْنِي . قَالَ يَا رَبِّ وَكَيْفَ أُطْعِمُكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ . قَالَ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّهُ اسْتَطْعَمَكَ عَبْدِي فُلَانٌ فَلَمْ تُطْعِمْهُ أَمَا عَلِمْتَ أَنَّكَ لَوْ أَطْعَمْتَهُ لَوَجَدْتَ ذَلِكَ عِنْدِي . يَا ابْنَ آدَمَ اسْتَسْقَيْتُكَ فَلَمْ تَسْقِنِي . قَالَ يَا رَبِّ كَيْفَ أَسْقِيكَ وَأَنْتَ رَبُّ الْعَالَمِينَ. قَالَ اسْتَسْقَاكَ عَبْدِي فُلَانٌ فَلَمْ تَسْقِهِ أَمَا إِنَّكَ لَوْ سَقَيْتَهُ وَجَدْتَ ذَلِكَ عِنْدِي)) مسلم
“Amesimulia Abu Huraira (r.a), “Amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) hakika Mwenyezi Mungu S.W atasema siku ya kiyama. Ee mwanadamu, nilikuwa mgonjwa lakini hukuja kuniona. Atasema: Ee Bwana wangu, nitawezaje kukutembelea ikiwa wewe ni Bwana wa ulimwengu? Allah atasema, je hukujua kwamba mja wangu huyu na yule alikuwa mgonjwa lakini hukuenda kumtembelea? Na je hukulifahamu hili kwamba kama ungemtembelea ungenikuta mimi kwake? Ee mwanadamu, nilikuomba chakula lakini hukunilisha. Naye atasema, Bwana wangu nitawezaje kukulisha hali wewe ni Bwana wa ulimwengu? Atasema Mwenyezi Mungu, Je hukujua kwamba mja wangu huyu na yule alikuomba chakula lakini hukumlisha? Je hukufahamu kwamba, kama ungemlisha ungenikuta mimi kando yake? Allah atasema tena, Eee mwanadamu, nilikuomba maji lakini hukunipa. Naye atasema, Eee Bwana wangu ningewezaje kukupa wewe maji nawe ni Bwana wa ulimwengu? Allah atasema, mja wangu huyu na yule alikuomba maji lakini, na kama ungemnywesha maji, ungenikuta mimi karibu yake” Sahihi Muslim Kitabu 32 Hadith Namba 6232
Linganisha na maneno haya ya Yesu ndani ya Biblia
“Mwana wa Adamu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote watakatifu pamoja naye, ndipo atakapoketi juu ya kiti cha enzi cha utukufu wake. Mataifa yotewatakusanyika mbele zake, naye atawatenga kama mchungaji anavyotenga kondoo na mbuzi.Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wake wa kushoto. Ndipo Mfalme atawaambia wale walioko upande wake wa kuume, ‘Njoni, ninyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini Ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. 35Kwa maana nilikuwa na njaa mkanipa chakula, nilikuwa na kiu mkaninywesha, nilikuwa mgeni mkanikaribisha, 36nilikuwa uchi mkanivika, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea.’Ndipo wale wenye haki watakapomjibu wakisema, ‘Bwana, ni lini tulikuona una njaa tukakulisha au ukiwa na kiu tukakunywesha?Lini tulikuona ukiwa mgeni tukakukaribisha au ukiwa uchi tukakuvika? Tena ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa tukakutunza au ukiwa kifungoni tukakutembelea?’ “Naye Mfalme atawajibu, ‘Amin, amin ninawaambia, kwa jinsi mlimvyotendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea Mimi.’Kisha atawaambia wale walio upande Wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu, ninyi mliolaaniwa, nendeni kwenye moto wa milele alioandaliwa kwa ajili ya ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa hamkunipa chakula, nilikuwa na kiu hamkuninywesha, 43nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha, nilikuwa uchi hamkunivika, nilikuwa mgonjwa hamkunitunza na nilikuwa gerezani nanyi hamkuja kunitembelea.’Ndipo wao pia watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, au ukiwa mgeni au uchi , au ukiwa mgonjwa na kifungoni na hatukukuhudumia?’Naye atawajibu, ‘Amin, amin nawaambia, kwa jinsi ambavyo hamkumtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu walio wadogo, hamkunitendea mimi.’Ndipo hawa watakapoingia kwenye adhabu ya milele, lakini wale wenye haki wataingia katika uzima wa milele” Mathayo 25:31-46.
Muhammad alifundisha Sala ya Bwana kwa wafuasi wake.
حَدَّثَنَا يَزِيدُ بْنُ خَالِدِ بْنِ مَوْهَبٍ الرَّمْلِيُّ، حَدَّثَنَا اللَّيْثُ، عَنْ زِيَادِ بْنِ مُحَمَّدٍ، عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ كَعْبٍ الْقُرَظِيِّ، عَنْ فَضَالَةَ بْنِ عُبَيْدٍ، عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ، قَالَ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ » مَنِ اشْتَكَى مِنْكُمْ شَيْئًا أَوِ اشْتَكَاهُ أَخٌ لَهُ فَلْيَقُلْ رَبُّنَا اللَّهُ الَّذِي فِي السَّمَاءِ تَقَدَّسَ اسْمُكَ أَمْرُكَ فِي السَّمَاءِ وَالأَرْضِ كَمَا رَحْمَتُكَ فِي السَّمَاءِ فَاجْعَلْ رَحْمَتَكَ فِي الأَرْضِ اغْفِرْ لَنَا حُوبَنَا وَخَطَايَانَا أَنْتَ رَبُّ الطَّيِّبِينَ أَنْزِلْ رَحْمَةً مِنْ رَحْمَتِكَ وَشِفَاءً مِنْ شِفَائِكَ عَلَى هَذَا الْوَجَعِ فَيَبْرَأُ »
“Imepokelewa kutoka kwa Abu Darda: amesema, ‘nilimsikia mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) akismea ‘ikiwa mmoja wenu anaumwa ugonjwa wowote, au ndugu yake anaumwa, basi na aseme, Bwana wetu ni Allah aliyeko mbinguni, Jina lako ni Takatifu, amri zako zatawala mbinguni na duniani, kama rehema zako zilivyo mbinguni utujaalie rehema hapa duniani. Utusamehe dhambi na makosa yetu, wewe ni Bwana wa watu wema. Tuma rehema kutokana na rehema zako na uponyaji kutokana na ponyo lako, ili kwamba ugonjwa huu uweze kupona.” Sunan Abu Daud Hadithi na. 3892
Shahidi wa Nne: Historia inathibitisha kwamba Biblia haijawahi kuharibiwa
Mwanahistoria Flavius Josephus (Karne ya Kwanza) akiandika katika mwaka wa 90 alitaja vitabu 24 vilivyokusanya historia ya Wayahudi ya kila ambacho kiliaminika kama Uvuvio.
Vitabu 5 vilindikwa na Musa, Vitabu 13 viliandikwa kati ya Musa na Mfalme Atashasta (Artaxerxes) wa Waajemi. Vitabu 4 vilikuwa vimejumuisha mashairi (vitabu vya Mashairi) na Nyimbo, Zaburi, Methali, Mhubiri, Maombolezo (Against Apion 1:38-40)
Kisha Josephus akaendelea kusema
“Ni kweli kwamba historia yetu imekuwa ikiandikwa toka wakati wa Atashasta, lakini maandiko hayo hayajachukuliwa kuwa ni maandiko sawa na maandiko ya kale ya mababu zetu. Hii ni kwa sababu, hakuna mfuatano wa manabii toka wakati huo. Na ni kwa kiasi gani tumekuwa na msimamo mkali na kuyaenzi maandiko hayo na kuchunga asije mtu akaongeza katika maandiko—Toka wakati huo, haijawahi kutokea mtu kuongeza maandiko hayo au kupunguza au kufanya badiliko lolote ndani yake.” (Against Apion 1:38-40)
Wayahudi hadi kufikia mwaka wa 100 AD walikuwa na uhakika kabisa kwamba vitabu vya manabii kama walivyopokea toka kwa Mwenyezi Mungu viko sahihi na havijawahi kuchafuliwa ama kutiwa mikono kama watu wengine wanavyotaka kutuaminisha siku hizi.
Shahidi wa Tano: Uvumbuzi wa Mabaki ya kale
Magombo kando ya Bahari mfu (Dead sea Scrolls)
Mnamo mwaka 1947 kijana mmoja wa Kiarabu aliyekuwa akichunga kondoo, alipoteza kondoo wake mmoja. Katika harakati za kumtafuta alianza kutupa mawe katika pango lililokuwa mlimani, ndipo aliposikia sauti mfano wa kuvunjika kwa vyungu. Kisha akamwita mchungaji mwenzie waliyekuwa wakisaidiana naye. Wote wawili waliingia katika pango hili ambamo ndani yake walikuta mitungi ya vyungu vyenye urefu wa inchi 25 hadi 29 na upana wa inchi 10. Ndani yake waliona Magombo ya ngozi yaliyovingilishwa. Vijana hawa walidhani ya kwamba wameokota hazina zilizositirika na hivyo walianza kutembea mjini Yerusalemu kutafuta wateja bila mafanikio. Ndipo walipofanikiwa kuyauza kwa Padre Athanasius Samweli wa Kanisa la Watawa wa Mt Mariko wa Orthodox Syria. Magombo mengine waliyauza kwa Dr. John C. Trever Mkurugenzi wa American School of Oriental Research. (TheThompson chain Reference Bible, Fifth Improved Edition uk. 1740)
Baadaye eneo hili lilifanyiwa uchunguzi na wataalamu wa mambo ya kale, uchimbaji na utafiti ulifanyika zaidi na kugundua magombo zaidi ya 800 katika eneno hili. Utafiti zaidi ulionyesha kuwa magombo haya yaliachwa pale tokea karne ya 1 (Mwaka 100AD) na Wayahudi wa kundi la Wa-Esene. Hawa inasadikiwa kuwa walikuwa wayahudi wenye msimamo mkali waliojitenga kutoka kwa wayahudi wengine ili kuepuka uchafu na ufisadi wa kidini uliofanywa na Wayahudi waliomwasi Mwenyezi Mungu. Wao waliamini kwamba wameitwa na Mungu kuitengeneza njia ya Bwana na kuyanyosha mapito yake. Yohana Mbatizaji anadaiwa kuwa alikuwa miongoni mwa watu wa kundi hili.
Utafiti wa magombo yote yaliyogunduliwa toka mwaka 1947 hadi mwaka 1952 umeonyesha kuwa karibia vitabu vyote 66 kama tulivyonavyo leo kwenye Biblia vimepatikana katika magombo mbalimbali. Hii inatoa ushahidi mwingine kwamba hakuna andiko lolote lililopotea ama kuharibiwa katika Biblia. Neno linasema “Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema kuliangalia kwa bidii kama vile nuru inayong’aa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi itokee mioyoni mwenu” 2Petro 1:19
Rafiki yangu napenda kukutia moyo endelea kuisoma Biblia yako ukiwa na uhakika kwamba, unashikilia mkononi mwako, MANENO YA MWENYEZI MUNGU ALIYE HAI, yaliyonenwa kupitia vinywa vya manabii wake. Tembea kifua mbele na uhakika kwamba, neno hilo lililoandikwa humo ni kama lilivyotoka kwa Mwenyezi Mungu tokea wakati wa manabii hao hadi sasa. Iamini Biblia kama kiongozi wako katika maisha ya kiroho na kwamba “ndani yake mna uzima wa milele”. Yohana 5:39